Rais wa TAHLISO aingilia kati changamoto ya malipo ya ada DIT

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:32 PM Jul 01 2025
Ziara ya Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, katika Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Picha:Mpigapicha Wetu
Ziara ya Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, katika Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, amefanya ziara ya kikazi katika Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kufuatia taarifa za ucheleweshaji wa malipo ya ada uliokuwa ukiwahusu baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho.

Taarifa zilizowasilishwa kwa TAHLISO zilieleza kuwa menejimenti ya DIT ilikuwa imetoa maelekezo ya kuwazuia wanafunzi waliochelewa kulipa ada kuingia katika mfumo wa kupata namba ya malipo, hatua iliyowafanya washindwe kusajiliwa rasmi na hivyo kuhatarisha ushiriki wao katika mitihani ya mwisho wa muhula (Final Exams - FE).

Katika ziara hiyo iliyofanyika leo Julai 1,2025 Rais Kiliba amekutana na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa DIT wakiongozwa na Rais wao, Bwana Mlade. Viongozi hao wameeleza kwa kina namna agizo hilo lilivyowaathiri wanafunzi wa kipato cha chini, ambao walikuwa bado wanahangaikia kumalizia ada zao.

Baada ya maelezo hayo, Rais wa TAHLISO amezungumza moja kwa moja na uongozi wa chuo hicho kwa lengo la kutafuta suluhu ya haraka na yenye kuzingatia utu. Katika mawasiliano hayo, aliomba chuo kutoa nafasi ya nyongeza ya muda kwa wanafunzi husika ili waweze kukamilisha malipo yao na kushiriki mitihani.

Kwa mshikamano na busara, uongozi wa DIT ulikubali ombi hilo na kutoa nafasi ya mwisho ya siku mbili kwa wanafunzi hao, hatua ambayo imepokelewa kwa shukrani kubwa na wanafunzi waliokuwa katika hatari ya kukosa mitihani.

TAHLISO imepongeza uongozi wa DIT kwa kusikiliza kilio cha wanafunzi na kuchukua hatua zenye kuzingatia maslahi ya elimu ya juu nchini. Pia imetoa pongezi kwa Serikali ya Wanafunzi wa DIT kwa kuonesha ushirikiano na uwajibikaji katika kutetea haki za wenzao.

Akihitimisha ziara hiyo, Rais Kiliba amezitaka taasisi zote za elimu ya juu nchini kuhakikisha changamoto zinazowakumba wanafunzi zinashughulikiwa kwa njia ya mazungumzo, usikivu na uelewa, ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa haki ya msingi ya elimu kwa sababu ya matatizo yanayoweza kutatuliwa kwa pamoja.