Ni Baraza Wawakilishi la kihistoria lililoongozwa na kinamama wawili

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 01:13 PM Jul 02 2025
Wajumbe wanawake wa baraza na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, baada ya kuliahirisha wiki iliyopita
PICHA: BWW
Wajumbe wanawake wa baraza na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, baada ya kuliahirisha wiki iliyopita

BAZARA la Wawakilishi linakaribia ukomo, likibakiza wiki mbili kuhitimishwa na kufungwa rasmi baada ya kuwatumikia Wazanzibari kwa miaka mitano.

Litafikia ukomo Agosti 13, limeandika historia kwa kuongozwa na Katibu mwanamama Raya Issa Mselemu, anayeshika nafasi hiyo kwa mara ya kwanza, kumbukumbu  zikionesha kuwa wadhifa huo ulishikiliwa na wanaume tangu  kuanza kwa utaratibu wa katibu mwaka 1982,  wa kwanza akiwa  Abubakar Khamis Bakari (marehemu).

Tangu kuanzishwa kwa BW limeongozwa na  makatibu tisa kati ya hao wanane ni wanaume na mwanamke mmoja  anayelihitimisha baraza hilo la 10 mwaka huu.

Bara  lenye wajumbe 77 kati ya hao 29 ni wanawake na 48 ni wanaume ambapo wanawake nane ndiyo waliochaguliwa majimboni huku wanaume  42 waliochaguliwa majimboni kati ya majimbo 50 ya uchaguzi Zanzibar mwaka 2020.

Baada ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuhutubia BW akiahirisha vikao vyake wiki iliyopita, wanasiasa wanatoa maoni yao, akiwamo  Naibu Spika  ambaye pia ni mwanamama Mgeni Hassan Juma, anayesema katibu huyo amesimamia kikamilifu masuala ya usawa wa jinsia.

Anafafanua kuwa kasi na nguvu ya wanawake ilikuwa kubwa katika baraza hilo na licha ya idadi ndogo ikilinganishwa na wajumbe wanaume lakini wameonyesha wana uwezo mkubwa wa kujadili na kuchambua hoja.

Anasema hata katika masuala ya sheria wanawake wanajadili na ajenda yao kubwa ni nafasi ya mwanamke ipo wapi katika sheria ambapo ni jambo muhimu ili kuongeza upeo wa uongozi kwa mwanamke pamoja na mambo mengine ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Anasema katika baraza hilo la 10, wanawake walikuwa mahiri  kuuliza masuala na wanafahamu vitu vingi hivyo mchango wa mwanamke umekuwa mkubwa na hata katika baraza hilo ambapo hata katika kamati za baraza wanafanyakazi kwa weledi mkubwa.

“Kwa mfano Kamati ya Bajeti Mwenyekiti ni mwanamke ambae pia ni mwakilishi wa jimbo la Dimani Mwanaasha Khamis, kwa hivyo bajeti imesimamiwa kwenye upande wa kijinsia kuona wanawake wanafaidika vipi katika bajeti ya serikali, ”anasema.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Wanawake (UWAWAZA) Dk. Saada Mkuya Salum, anasema awali katika baraza hilo kuna sheria nyingi zilikuwa zinapita lakini hazina muangalizi wa masuala ya kijinsia lakini wanawake wamekuwa vinara wa kuzingatia masuala ya jinsia.

Dk. Saada Waziri wa Fedha na Mipango, anasema kuwa hata bajeti ya serikali ya mwaka 2025/2026 imezingatia masuala ya kijinsia ili kuhakiksiha fedha zinazotengwa zinayanufaisha makundi yote ya wanawake na wanaume.

“Kwa mara hii UWAWAZA tulisema tusikae ndani tu kujifungia lazima tushirikiane na wadau wengine kuwawezesha wanawake kisiasa, kujenga uwezo wao na sisi kuwa vinara kwa wanawake wengine kuweza kuingia katika milengo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi,”anaongeza Saada.

Aidha, anasema wanataka kuona mfumo wa kishehia unaozingatia mfumo wa kijinsia ili majukwaa ya kijinsia kuanza katika ngazi ya shehia na kuwajenga wanawake kuwa na mawazo ya kujiimarisha kiuchumi na kisiasa.

Dk. Saada anamzungumzia Katibu wa Baraza Raya kuwa ni msaada mkubwa katika kuzingatia masuala ya kijinsia na alisimamia kuhakikisha kuna miundombinu rafiki katika baraza hilo kwa jinsi zote bila  vikwazo.

“Ametusaidia sana kwa kuwa na mwamko wa kijinsia maana katibu Raya pia ni sehemu ya wajumbe wa UWAWAZA na amekuwa msaada mkubwa kwetu, mfano miaka yote tangu baraza hili kujengwa lilikuwa halina miundombinu rafiki kwa wenye ulemavu lakini amelisimamia hilo na hivi sasa ipo miundombinu ya kuhakikisha wana uwezo wa kufika katika vikao vyetu vya baraza,”anasema.

Riziki Pembe, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, anasema Katibu wa Baraza la Wawakilishi alikuwa karibu katika kutoa mchango kwa wanawake akisaidia  katika kufahamu mambo mbalimbali ya kisheria kwa sababu kitaalamu pia ni mwanasheria.

“Ametusaidia sana katika miswada mbalimbali . Wanawake tunaifahamu vizuri na kuwa na uwezo wa kuchangia na kujenga hoja inapowasilishwa barazani,”anasema.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wa wajumbe wa baraza hilo, anasema wabunge wanawake walifanya vizuri katika baraza hilo na hilo limetoka na kujengewe uwezo na UWAWAZA.