KIFO EDGAR LUNGU; Kukiuka katiba kwauacha mwili wake mochwari Pretoria

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:25 PM Jul 02 2025
Edgar Lungu, kifo chake kimesababisha bmgogogro familia na serikali
Picha: Mtandao
Edgar Lungu, kifo chake kimesababisha bmgogogro familia na serikali

NI takriban mwezi tangu Edgar Lungu ((68), Rais wa sita wa Zambia, kufariki dunia huko Pretoria Afrika Kusini, lakini hajazikwa, kwa vile familia inataka kuzikwa ugenini kinyume na katiba yao inayoelekeza mazishi ya kijeshi kwa heshima zote za kiserikali. Kisa cha mkanganyiko huo ni chuki dhidi ya serikali.

Katiba inaelekeza maziko yaongozwe na rais aliyeko madarakani na yafanyike kwa taratibu za kijeshi na kiserikali kama heshima ya utumishi wake kwa taifa.

Akitwaliwa Juni 5, Lungu anaacha majonzi na kutonesha upya kidonda cha kisiasa kilichozungukwa na chuki zisizoisha, baada ya familia yake kuamua azikwe Afrika Kusini na kuendeleza mzozo wa kisiasa kati yake Rais Hichilema, aliyeko madarakani.

Ni uamuzi usio wa kawaida kwa kiongozi wa kitaifa kama Lungu kuzikwa nje ya ardhi aliyoiongoza, jambo linaloibua maswali magumu kuhusu migawanyiko ya kudumu ya kisiasa.

CHANZO CHA MPASUKO

Mzozo kati ya Lungu na Hichilema, ulianza mwaka 2016, marehemu huyo akiongoza kutoka chama cha Patriotic Front (PF), alitangazwa mshindi dhidi ya mpinzani Hichilema kutoka United Party for National Development (UPND).

Hata hivyo, matokeo hayo yalizingirwa na madai ya wizi wa kura na udanganyifu. Hichilema alikataa kuyakubali, akiyaita ni mamlaka yake yaliyoporwa, ukawa msingi wa uhasama na siasa za mgawanyiko wa karibu muongo mmoja sasaa.

Aprili 2017, mvutano ulishika kasi baada ya magari ya Hichilema kudaiwa kukataa kumpisha msafara wa Rais Lungu.Tukio hilo lilisababisha Hichilema kukamatwa na kushtakiwa kwa uhaini, shitaka lisilo na dhamana, aliwekwa kizuizini kwa zaidi ya siku 120.

Jumuiya ya kimataifa ililaani, Shirika la Msamaha wa Wafungwa Amnesty International likimtangaza kama ‘mfungwa wa dhamira’.

Serikali ya Lungu ilitetea hatua hiyo kuwa ni kulinda usalama wa taifa, lakini wengi waliiona ni njama za kuzima upinzani. Baada ya kuachiliwa kwa Hichilema, hakukuwa na dalili ya maridhiano kati yao. Kwa miaka mingi, Hichilema alikataa kumtambua Lungu kama ‘Rais’, akisisitiza kuwa hakuchaguliwa kihalali. Uhasama huu ulienea hadi kwenye jamii, na kuchochea mgawanyiko wa raia. 

UCHAGUZI WA 2021

Agosti 2021, Wazambia walipiga kura wakitaka mabadiliko, Hichilema akashinda kwa zaidi ya asilimia 60 dhidi ya Lungu, japo makabidhiano ya serikali yalifanyika kwa heshima, mvutano wao ulizidi.

Lungu alijitenga na siasa kwa muda, hadi mwishoni mwa 2022 alianza kutoa matamko ya kisiasa akidai serikali mpya ilikuwa inawanyanyasa washirika wake wa zamani.

Serikali ya Hichilema ilimshutumu kuvunja sheria ya marupurupu ya marais wastaafu kwa kuendelea na siasa, marupurupu yake yakafutwa, ikiwemo ulinzi na nyumba ya serikali. Hatua hiyo, ilizidisha mvutano.

Lungu alidai kuwa alilazimika kuzungumza kwa niaba ya demokrasia ya Zambia. 

FAMILIA YABANWA

Mwaka 2023, mke wa Lungu, Esther, alishtakiwa kwa ununuzi wa ardhi kwa njia isiyo halali na utakatishaji wa fedha, watoto nao  walihusishwa na kuvunja sheria za forodha na kumiliki mali za kifahari.

Chama cha PF kililalamikia mashitaka hayo lakini serikali ikasisitiza hakuna aliye juu ya sheria.

Mwaka 2024, Mahakama ya Katiba ilitoa uamuzi wa kushangaza kwamba Lungu anaweza kugombea tena, ikibadili uamuzi wa awali na kuleta mshituko, hasa baada ya mabadiliko ya ghafla ya majaji wakuu, jambo lililoibua hofu kuhusu uhuru wa mahakama.

Kwa kuwa mahakama ilimuidhinisha, Lungu alianza kuashiria kurejea kwenye siasa, ingawa afya yake ilizidi kudorora akisumbuliwa na moyo.

KIFO A/KUSINI

Mwaka jana mwishoni iliripotiwa kuwa Lungu anaumwa moyo, na alihitaji matibabu maalumu ambayo hayakupatikana Zambia. Ukazuka mvutano mkubwa pale ilipodaiwa kwamba alinyimwa kibali cha matibabu nje ya nchi na serikali.

Hatimaye, kwa ufadhili binafsi, alikwenda Pretoria kutibiwa na ilipofika Juni 5, 2025, aliaga dunia.

Mara baada ya kifo chake, serikali ya Zambia ilitangaza maombolezo ya siku 10 na mipango ya maziko ya kitaifa. Hata hivyo, familia yake ilikataa.

Kupitia msemaji ilisema Lungu aliandika wosia kwamba hataki kuzikwa chini ya usimamizi wa serikali ya Hichilema na kutoa sababu za usalama, ukosefu wa imani na kutaka apumzike mahali pa amani.

Hivyo, alizikwa kwa faragha makaburi ya Westpark Afrika Kusini mnamo Juni 20, 2025, bila kuhusisha serikali ya Zambia.

Viongozi wa PF walihudhuria, lakini serikali ya sasa haikutuma wawakilishi huku Rais Hichilema akifupisha maombolezo kwa siku mbili. Akisema taifa linapaswa kuzingatia siku za usoni badala ya kushikilia yaliyopita, akisisitiza umoja wa kitaifa, wengine wakiona kauli hiyo kama ya kisiasa zaidi na isiyoonyesha hisia za taifa.

Kwa baadhi ya Wazambia, hasa wafuasi wake ilikuwa ni ishara ya mwisho ya kupinga mateso na dhihaka alizodai kupata. Kwa wengine, ni usaliti kwa taifa, kwani ilizua hofu ya kukosa maridhiano ya kitaifa.

Mitandaoni, Wazambia wanajadili kwa hisia kali, wengine wakilia, wengine wakifurahia. Mashirika ya kiraia yakitoa wito kwa viongozi kuachana na visasi vya kisiasa.

Mvutano kati ya Lungu na Hichilema haukuwa tu mgongano wa watu wawili, ulikuwa kioo cha changamoto za kisiasa na za kitaasisi nchini humo.

Maziko ya Lungu yamebeba maana kubwa zaidi, yanaonyesha madhara ya chuki za kisiasa zinazodumu hata baada ya maisha, pia yanaakisi hatari ya taifa kuendelea kugawanyika na umuhimu wa maridhiano ya kweli.

Swali linalobakia ni, je, Zambia inaweza kuzika tofauti zake na kujenga umoja wa kitaifa, au itaendelea kulia kwa makaburi yasiyo na alama ya maridhiano?

MOUNT KENYA TIMES