PURA, ZPRA zajivunia miaka mitatu ya mashirikiano

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:40 PM Jul 02 2025
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi, Charles Sangweni.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi, Charles Sangweni.

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ya Tanzania Bara na Mamlaka ya Uthibiti, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta Zanzibar (ZPRA) ya Zanzibar zimeeleza kujivunia mafanikio yaliyopatikana tangu taasisi hizo ziliposain Hati ya Makubaliano mwaka 2022.

Hayo yameelezwa Julai 01,  2025 Jijini Dar es Salaam katika kikao kilichohusisha menejimenti za PURA na ZPRA kwa lengo la kujadili taarifa ya utekelezaji wa MoU kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi, Charles Sangweni alisema kuwa tangu kuanza kutekelezwa kwa MoU, Taasisi za PURA na ZPRA zimefanikisha masuala mbalimbali ikiwamo kujengeana uwelewa katika eneo la udhibiti wa shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.

“Ni jambo la kujivunia kuona hali ya utekeleza wa MoU baina yetu umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka na tumeweza kufanikisha masuala mengi kupitia MoU hii” alisema Sangweni.


Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZPRA, Mhandisi. Mohammed Said alisema kuwa miaka mitatu ya MoU imekuwa na manufaa makubwa kwa taasisi hizo hususan katika eneo la kujengeana uwezo.

Tangu kusainiwa kwa MoU, PURA na ZPRA zimeweza kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo usimamizi wa data za petroli, ukaguzi wa gharama za uwekezaji na uandaaji wa sheria, kanuni na miongozo.

Maeneo mengine ni udhibiti na usimamizi wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli na ushiriki wa wananchi katika shughuli hizo.