JUMATANO iliyopita katika Kura Yangu Nguvu Yangu, tulibaini kwamba kukosa nguvu ya kiuchumi kunaathiri ushiriki wa wanawake katika siasa kwa kiwango kikubwa. Pia tulibaini kuwa changamoto hiyo imekuwa chanzo cha wanawake kutojitokeza kugombea au, kuogopa kuendelea na safari ya kisiasa, au kushindwa kushindana kwa usawa na wanaume.
Leo katika safu yetu, tutajikita katika kuangalia mbinu zipi zitumike kuwawezesha wanawake kiuchumi.Fuatana na Mwandishi Wetu, Joyce Bazira
Uwezeshaji kiuchumi utainua ushiriki wa wanawake katika siasa ili wanawake waweze kushiriki kikamilifu katika siasa, ni muhimu kuwepo kwa mifumo ya kuwasaidia kiuchumi. Ipo mitazamo mbalimbali kuhusu namna ambavyo mwanamke anaweza kusaidiwa ili kujiimarisha kiuchumi na hatimaye kuwa na uwezo kutekeleza mipango yake ikiwemo kushiriki harakati za kisiasa.
Wapo wanaoshauri kwamba iundwe mitandao ya biashara inayolenga kuwasaidia wanawake kuanzisha shughuli za kibiashara zinazoweza kuwaingizia kipato na pia kuwapa mafunzo wanawake juu ya mambo ya kifedha ili waweze kuendesha shughuli zao kwa faida na kwa ufanisi.
Wanaounga mkono mtazamo huu wanasema, mwanamke akiwa na rasilimali zake mwenyewe atakuwa na uhuru wa kuamua kitu gani akipe kipaumbele katika matumizi yake.
Wanasema njia nyingine za kumsaidia mwanamke ikiwa ni pamoja na kuchangiwa fedha na familia, marafiki au watu wengine, wakati anapoamua kuingia kwenye siasa, zimekuwa siyo endelevu.
Baadhi ya wanawake wanasiasa waliozungumza na mwandishi wa safu hii kwa nyakati tofauti, wanakiri kwamba kupewa msaada wa kifedha na ndugu au marafiki, hasa unapowaeleza nia yako ya kuingia kwenye siasa, inakuwa ngumu na wengi badala ya kukusaidia, wanakukatisha tamaa.
Zipo ripoti mbalimbali zinazoonyesha jinsi changamoto za kiuchumi inavyowakwamisha wanawake nchini, kuwania uongozi. Kwa mfano, katika uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020, kulikuwa na taarifa kwamba wako wanawake wengi waliojiondoa kuwania nafasi za udiwani kwa sababu ya kutokuwa na fedha za kuendesha kampeni. Baadhi walikiri kushindwa kumudu gharama za usafiri, chakula kwa mawakala wao, na kuchapisha mabango ya kampeni.
Kukosa nguvu ya kiuchumi huwafanya wanawake wadharauliwe. Katika jamii nyingi, umaskini huendeleza mitazamo ya kijinsia inayoweka wanawake nyuma kisiasa. Ipo mifano inayoonesha namna wanawake wanavyonyimwa nafasi kwa sababu tu ya hali yao ya kiuchumi, na siyo uwezo wao wa kiuongozi.
Aidha, wanawake wanaotoka katika familia au maeneo yenye umaskini hupata changamoto zaidi za kujikubali kama viongozi kutokana na ukosefu wa motisha na kuungwa mkono. Wanapojaribu kugombea nafasi za kisiasa, hukumbana na kauli za kudhalilisha, kudharauliwa, au kuambiwa siasa si za wanawake maskini.
Ubaguzi wa kijinsia unaochochewa na umaskini huendeleza mfumo usio wa haki ambao unawanyima wanawake fursa ya kushiriki siasa kwa usawa. Ili kuvunja mnyororo huu, ni muhimu kuwekeza katika elimu, uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake, na kuondoa mitazamo ya kijinsia inayowatenga kwenye uongozi.
Iko mifano mingi inayoonyesha namna ambavyo wanawake wenye mafanikio ya kiuchumi wanavyopata heshima na kutambulika zaidi. Hali hii si tu kwamba huwajengea kujiamini bali pia huvunja kuta za mitazamo potofu inayosema kuwa uongozi ni kazi ya wanaume pekee.
Wanawake wenye ushawishi wa kiuchumi wanaonesha kwa vitendo kwamba wanaweza kuongoza kwa ufanisi na kuleta mabadiliko chanya.
Uwezo wa kiuchumi hutoa fursa kubwa kwa wanawake kupata wafuasi na washirika, ambao ni nguzo muhimu katika siasa za kisasa. Wanapopata heshima, wanawake wanapata urahisi wa kuingia kwenye meza za maamuzi, na hivyo kuongeza ushawishi wao si tu kwa ajili yao wenyewe, bali kwa jamii nzima.
Kadhalika uwezo wa kiuchumi huwapa wanawake uhuru wa maamuzi. Katika jamii zetu, wanawake wengi bado wanakosa nafasi ya kushiriki siasa kwa sababu wanategemea wengine kwa mahitaji yao ya msingi.
Hali hii huwafanya waogope kujitokeza kwa sababu ya hofu ya kupoteza riziki au kukataliwa na wale wanaowategemea. Lakini mwanamke anapojitegemea kiuchumi, anakuwa huru kusema ukweli, huru kusimamia maamuzi yake, na huru kusimama kwa ajili ya maslahi ya watu wake.
Mwanasiasa anayejitegemea hana haja ya kushinikizwa na wafadhili au makundi yenye masharti. Anaweza kushiriki mijadala ya kisiasa kwa msimamo, kwa uhuru wa fikra, na kwa dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko. Huu ndio uongozi tunaoutamani uongozi wa heshima, wa maadili na wa kujitolea.
Kwa hiyo, tukitaka kuona wanawake wakijitokeza kwa wingi kwenye siasa, ni lazima tuwekeze katika kuwawezesha kiuchumi. Tukiwapa wanawake zana za kujitegemea, tutakuwa tumewapa silaha ya kupaza sauti zao, kushiriki maamuzi, na kuchukua nafasi zao za haki katika uongozi wa taifa letu.
Kampeni kuhamasisha ushiriki wa wanawake kwenye siasa ziende sambamba na uwezeshaji wa kiuchumi. Hili linaweza kutekelezwa kwa kuweka mikakati itakayowawezesha wanawake kupata mitaji na mikopo yenye masharti nafuu. Mwanamke mwenye biashara au mradi ana nafasi kubwa ya kujitegemea kifedha na hivyo kushiriki kwenye siasa bila utegemezi.
Pili, mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa fedha yanahitajika. Wanawake wakielimishwa jinsi ya kuendesha biashara na kusimamia fedha zao, wanajenga misingi imara ya kujisimamia kiuchumi na kujitokeza kwenye uongozi.
Tatu, tunapaswa kuhakikisha wanawake wanamiliki ardhi na mali, kwani mali ni nyenzo muhimu ya kujipatia mikopo na kujiinua kiuchumi. Bila haki ya umiliki, wanawake hubaki nyuma, wakiwa wanyonge mbele ya mifumo ya kifedha.
Pia tusisahau umuhimu wa kuwa na mifumo inayowapunguzia wanawake mzigo wa majukumu ya nyumbani na kuwapa nafasi ya kushiriki kwenye shughuli za maendeleo, ikiwemo siasa.
Ili kuongeza ushiriki wa wanawake, ni muhimu kuweka sera na mipango ya kuwawezesha kiuchumi, kutoa mafunzo, na kuunda mazingira ya usawa wa kijinsia katika uongozi.
Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha wanawake wanapata nafasi na nguvu za kiuchumi zinazowawezesha kutambuliwa na kuwa kishawishi, licha ya kuleta usawa wa kijinsia katika uongozi, itakuza demokrasia imara.
Swali la kufikirisha:
Nini kifanyike kuwawezesha wanawake kiuchumi?
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED