ACT Wazalendo yasema serikali imeshindwa kumaliza umasikini

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 02:37 PM Jul 04 2025
Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Chama cha ACT Wazalendo kimewataka Watanzania kuwahoji na kuwapima watawala kwa msingi wa utekelezaji wa Katiba, hususan kifungu cha kupunguza umasikini wa wananchi, badala ya kuridhika na maneno ya kisiasa yasiyo na uhalisia wa maisha ya kila siku.

Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe, katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Inyonga, wilayani Mlele mkoani Katavi, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya ACT Wazalendo inayoitwa Operesheni Majimaji – Linda Kura Yako.

"Tulifanya uchaguzi mwaka 2020, sasa tunaelekea uchaguzi mwingine. Ni wakati wa kujiuliza: serikali iliyopo madarakani imetekeleza vipi ibara ya 9(i) ya Katiba? Baada ya uchaguzi wa mwaka 2020, Watanzania milioni 14 waliishi chini ya mstari wa umasikini. Leo hii, mwaka 2024, idadi hiyo imefikia milioni 26 – watu wanaoshindwa kupata hata Sh 1,600 kwa siku," alieleza Zitto, ambaye pia ni mchumi kitaaluma.

Amesema kuwa licha ya viongozi wa serikali kuendelea kusema "Mama ameshusha mabilioni," hakuna mahali popote ambapo wameweza kuonesha wazi kuwa kiwango cha umasikini kimepungua miongoni mwa wananchi.

Zitto amedai kuwa sera zinazotekelezwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) hazijafanikiwa kuondoa umasikini, hali inayoendelea kuwaathiri Watanzania wengi, hasa walioko maeneo ya pembezoni. "Kwa sababu hiyo, tunawaomba Watanzania watuunge mkono kuiondoa CCM madarakani," alisema.

Ameongeza kuwa kipindi pekee ambapo umasikini ulianza kupungua ni wakati ambapo kulikuwa na vyama vya upinzani vilivyo imara bungeni, waliokuwa wakiihoji serikali na kuisimamia kwa karibu, hali ambayo kwa sasa haitokei tena kutokana na Bunge kuwa la chama kimoja.

Kwa mujibu wa Zitto, mikoa ya Kanda ya Magharibi ikiwemo Tabora, Rukwa, Kigoma na Katavi inaongoza kwa kiwango cha umasikini, hali inayodhihirisha tofauti kubwa ya kiuchumi kati ya walio nacho na wasio nacho.

"Hii ni ishara kwamba kuna tatizo la msingi katika namna ya ugawaji wa rasilimali na utekelezaji wa sera za maendeleo. Hatupaswi kukubali hali hii iendelee," alisisitiza.