Karia akosa mpinzani kinyang'anyiro urais TFF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:03 PM Jul 04 2025
news
Picha Mtandao
Mgombea wa nafasi ya urais TFF Wallace Karia.

Katika hatua ya kuwatafuta wagombea urais Kamati ya Uchaguzi ya TFF imewang'oa wagombea watano wa nafasi ya Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kubaki na jina moja pekee la Wallace Karia aliyekuwa rais wa shirikisho hilo

Akitoa taarifa ya usahili wa uchaguzi huo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF Wakili Kiomoni Kibamba, amesema Karia ndiye mgombea pekee aliyekidhi vigezo kwa mujibu wa kanuni na kama kuna mtu anapingamizi bado ana nafasi ya kukata rufaa.

Kibamba amesema wagombea wengine wanne kati ya sita. wamekosa sifa za kukidhi kanuni za uchaguzi na kwamba mgombea mmoja alishindwa kutokea kwenye usahili.

"Kwenye nafasi ya urais kulikuwa na wagombea sita, mmoja hakutokea kwenye usahili na wengine wanne hawakukidhi matakwa ya kikanuni, mgombea mmoja amekidhi matakwa yote na tumempitisha ambaye ni Wallace Karia," amesema Kibamba.

Wakili Kibamba amesema kuwa kwenye nafasi ya wagombea wa nafasi ya ujumbe kulikuwa na wagombea 19 ambapo 17 walihudhuria usahili, saba wamekosa vigezo na 10 wamepitishwa kuendelea na mchakato wa uchaguzi katika hatua inayofuata.

Pia Wakili Kibamba amesema wagombea ambao wamekosa sifa na kukatwa, wana nafasi ya kwenda kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya uchaguzi endapo wataona hawajatendewa haki.

"Sisi ni kamati ya uchaguzi na ni binadamu inawezekana wapo ambao wataona wameonewa wana nafasi ya kwenda kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi, wakiturudishia jina lake siai hatuna shida tutalipokea na kuendelea na uchaguzi," amesema Kibamba.