Vijana waipongeza serikali mazingira bora ya uwekezaji

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:04 AM Jul 05 2025
Joseph Mwakalinga (kulia) na Amani Hamis
Picha: Christina Mwakangale
Joseph Mwakalinga (kulia) na Amani Hamis

VIJANA waliopata nafasi ya kufanya kazi katika kampuni za kigeni zilizowekeza Tanzania, wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuweka mazingira rafiki ya kuvutia wawekezaji.

Wakizungumza na Nipashe Digital, katika viwanja vya Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF), vijana hao wanasema uwapo wa sera nzuri ambazo zimewavutia wawekezaji ndizo zimechangia na wao kupata fursa ya ajira kupitia wawekezaji hao ambao wamewekeza nchini. 

Wanasema endapo serikali isingeweka sera nzuri huenda wawekezaji hao wasingekuja kuwekeza na wao wasingepata fursa ya ajira kama walivyopata sasa.

Joseph Mwakalinga, ni Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya kutoka nchini China ya Weichai, anasema uamuzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha mazingira ya uwekezaji kuwa rafiki, amewakomboa vijana wengi kupata ajira katika kampuni na miradi mbalimbali ya uwekezaji inayowekezwa na watu kutoka ndani na mataifa ya nje.

"Hata katika kampuni hii ambayo imetuajiri sisi, wanafurahia sana mazingira ya uwekezaji yalivyoimarishwa na serikali ya awamu hii ya sita, wakati wanakuja kuwekeza walikuwa na wafayakazi watatu tu lakini kwa sasa tupo 45 na kati ya hao wageni wako wawili tu na wengine wote ni Watanzania.

"Hii yote ni fursa kwetu kwa sababu serikali yetu inanufaika na uwapo wa wawekezaji lakini na sisi wananchi mmoja mmoja tunanufaika pia, ina maana mazingira ya kuwekeza yangekuwa mabovu wasingekuja na sisi tusingepata ajira, kwa hiyo sisi tunaishukuru sana serikali yetu," amesema Mwakalinga.

"Hivyo, mimi nawaomba Watanzania wenzangu tuendelee kuijega nchi yetu na kuunga mkono kazi kubwa inaofanywa na serikali yetu."

Amani Hamis, mfanyakazi wa kampuni hiyo, anasema kabla ya kuajiriwa katika kampuni hiyo, alikuwa anafanya vibarua ambavyo kipato alichokuwa akikipata hakikutosheleza mahitaji yake na familia yake lakini kwa sasa kipato anachopata kimemfikisha katika hatua nzuri kimaisha. 

"Zamani sikuwa na uwezo hata wa kuendesha familia yangu, lakini kwa sasa tangu nipate ajira kwenye kampuni hii, maisha yangu ni mazuri, nasaidia hata ndugu zangu, nina kwangu na napatiwa huduma zote muhimu kutoka kwenye kampuni ikiwamo bima ya afya na NSSF.