Dar es Salaam kinara kuripoti migogoro Kituo Msaada Kisheria

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:53 PM Jul 04 2025
Msimamizi wa Kituo hicho, Judica Nkya
Picha: Mpigapicha Wetu
Msimamizi wa Kituo hicho, Judica Nkya

MIGOGORO ya mirathi na ardhi ndio inayoongoza kuripotiwa kwenye Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Kadhalika, mkoa wa Dar es Salaam ndio unaoongoza kwa kuripoti migogoro hiyo ukifuatiwa na Mkoa wa Njombe.

Kwa mujibu wa Msimamizi wa Kituo hicho, Judica Nkya, tangu kizinduliwe rasmi Septemba mwaka jana, tayari kimepokea migogoro 1508 na asilimia 66 kati yake zimefanyiwa kazi na kuhitimishwa na asilimia 34 iliyobaki inaendelea kushughulikiwa katika hatua mbalimbali. 

Nkya anasema kituo hicho hupokea migogoro au malalamiko kutoka kwa wananchi nchi nzima katika maeneo tofauti kwa njia ya simu na kuanza kufanyiwa kazi mara moja kwa ajili ya utatuzi kwa njia za kisheria. 

"Kituo kinahudumiwa na Wanasheria wabobezi ambao wanatoa huduma kwa wananchi katika kila pembe ya nchi kwa njia ya simu, ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani, njia ya kawaida pamoja na barua pepe,"amesema Nkya.

Pia, amesema kituo hicho kimeungaishwa na taasisi mbalimbali za serikali pamoja na za binafsi kwa ajili ya kuhudumia Wananchi katika maeneo mbalimbali. 

"Pamoja na kupokea malalamiko kwa njia za mtandao, pia Wizara na Kituo tunapokea mengine kwa njia ya barua ambazo zinatumwa kwa njia ya Posta au moja kwa moja wizarani na yanashughulikiwa kwa njia hiyo kupitia kituo cha huduma kwa mteja,"amesema Nkya. 

Amesema katika kutoa huduma hiyo kwa wananchi, wamegundua kwamb bado hakuna uelewa wa kutosha wa sheria kwa wananchi wengi hasa katika eneo la mirathi.

"Bado wananchi wengi hawajafahamu taratibu za kufungua kesi za kusimamia mirathi, kwa hiyo wanapopiga simu sisi tunawaelewesha na kuwaelimisha hatua za kisheria za kufuata," amesema Nkya.