Mimba za utotoni Iringa zapungua

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 03:46 PM Jul 04 2025
Mimba za utotoni Iringa zapungua
Picha:Mtandao
Mimba za utotoni Iringa zapungua

Shirika la SOS Children’s Village limefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya mimba za utotoni kwa wasichana mkoani Iringa, kutoka asilimia 18 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 15 mwaka 2024, kupitia utekelezaji wa mradi wa Mabinti Bora unaolenga kuimarisha malezi na elimu kwa watoto.

Mradi huo umefadhiliwa na Serikali ya Finland kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, na kuhusisha wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa serikali kutoka idara za elimu na maendeleo ya jamii.

Akizungumza katika kikao kazi cha kupitia sera za vijana na changamoto zake, Meneja wa Mradi huo, Victor Mwaipangu, alisema kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo, takwimu zilionesha asilimia 18 ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 18 walikuwa wakipata mimba za utotoni, hali iliyowapelekea wengi kushindwa kuendelea na masomo.

“Takwimu za kitaifa zinaonesha asilimia 22 ya wasichana hupata mimba za utotoni. Kwa Iringa tulianza na asilimia 18 lakini kwa sasa Manispaa ya Iringa imepungua hadi chini ya asilimia 10, huku wilaya za Mafinga na Mufindi zikiwa kwenye asilimia 10 na 12,” alifafanua Mwaipangu.

Amesema kupitia ushirikiano na walimu, maafisa wa maendeleo ya jamii na viongozi wa shule, waliweza kutoa elimu ya malezi, haki na wajibu wa watoto kwa wanafunzi, wazazi na walimu katika shule mbalimbali mkoani humo.

“Tulianza na matukio 36 ya mimba kwa mwaka, lakini sasa matukio hayo yamepungua hadi kufikia kati ya sita hadi nane kwa mwaka,” alisema.

Mbali na mradi wa Mabinti Bora, Mwaipangu alisema shirika hilo pia liliwahi kutekeleza mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuelimisha kuhusu haki za watoto, ambao uliwanufaisha wanawake 250 wa Mufindi waliokuwa wakilea watoto zaidi ya 1,000.

Pia walitekeleza mradi wa elimu katika shule nane wilayani Iringa uliolenga kuboresha miundombinu ya kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa vyoo na ukarabati wa madarasa, jambo lililopelekea baadhi ya shule zilizokuwa zikishika nafasi za mwisho kitaaluma, kupanda hadi nafasi ya tatu bora kwa ngazi ya wilaya.

Kwa upande wake, Afisa Mradi kutoka SOS Children’s Village, Benson Lwakatare, alisema kikao kazi hicho kilishirikisha maafisa kutoka Wizara ya Afya, Elimu, TAMISEMI, na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, pamoja na viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Lwakatare alieleza kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kupitia sera zilizopo zinazohusu vijana, kuangalia changamoto katika utekelezaji wake, na kutafuta njia bora za kuimarisha maisha ya vijana kupitia miradi yenye tija.

“Ni muhimu kuhakikisha sera zinaendana na uhalisia wa maisha ya vijana wetu, ili miradi tunayotekeleza iwe na matokeo chanya na ya kudumu,” alisisitiza.