Wakazi wa Kijiji cha Mtakuja kilichoko Kata ya KIA, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, ambao ni jamii ya wafugaji wa Kimasai, wameyatua 'mateso' ya muda mrefu ya kutembea kilomita 12, kufuata huduma za afya, nje ya kata hiyo.
Iliwachukua siku nzima kusotea matibabu nje ya kijiji chao, lakini sasa serikali imeboresha huduma za afya kwa kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Kituo cha Afya Kata ya KIA, chenye thamani ya Sh.milioni 209.6
Akitoa taarifa ya mradi huo, leo Julai 4, 2025 kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Alli Ussi, Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Dk. Itikija Msuya (DMO), amesema wananchi hao sasa wameondokana na adha hiyo.
Akizungumza na wananchi wa Mtakuja, kabla ya kuweka jiwe la msingi mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Ismail Ali Ussi , aliwataka waliopewa dhamana ya ujenzi wa kituo hicho kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati ili kuweze kuleta tija kwa jamii hiyo.
Amesema Rais, Samia Suluhu Hassan, ameamua kusogeza huduma za afya kwa wananchi, ambapo ameitaka serikali wilayani Hai, kuhakisha mradi huo unatekelezeka kwa wakati.
Pamoja na mambo mengine, kiongozi huyo wa mbio za mwenge kitaifa, amesisitiza kuwa uwekezaji katika afya, ni msingi wa maendeleo ya taifa, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika kulinda na kutunza miundombinu inayojengwa.
Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Bomboko, ameeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo umetokana na serikali kuwatafutia maeneo mapya wananchi waliokuwa wakiishi eneo linalomilikiwa na Kampuni ya Usimamizi na Uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), hivyo kusogeza huduma za afya kwao.
Miradi mingine, ni ujenzi wa shule mpya ya Msingi Kwa Sadala, mradi wenye thamani ya Sh.milioni 380,422,700, na ujenzi wa barabara ya Shabaha yenye urefu wa 0.59 inayojengwa kwa kiwango cha lami katika Kata ya Muungano, unaogharimu Sh.milioni 380,422,000.
Umo, mradi wa ujenzi wa jengo la biashara ya Kiriwe na matumizi ya nishati safi, Kata ya Bomang'ombe, lenye thamani ya Sh.milioni 756,299,713.
Kadhalika, mwenge huo umegusa mradi wa maji Kikafu Soka, Kwa Sadala, ambao una thamani ya Sh. milioni 997,100,000 na mradi wa vijana wa Saluni na Barbershop unaotokana na mikopo ya asilimia 10 katika Kata ya Bomang'ombe, ambao una thamani ya Sh. milioni 32,000.
Kadhalika, iko miradi ya ujenzi wa jengo la famasi,maabara,upanuzi wa wodi ya wazazi, wodi ya daraja la kwanza na njia ya kulitishia wagonjwa (walk Ways), uliogharimu jumla ya Sh. milioni 900,000,000.
Miradi hiyo, inafanya jumla ya miradi iliyokaguliwa,kuwekewa jiwe la msingi na kuzindua miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh.bilioni 3.631.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED