Serikali yapokea magari kwa Kampeni ya nishati safi ya kupikia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:33 PM Jul 04 2025
Serikali yapokea magari kwa Kampeni ya nishati safi ya kupikia
Picha:Mpigapicha Wetu
Serikali yapokea magari kwa Kampeni ya nishati safi ya kupikia

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Dk. Khatibu Kazungu, amesema ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya dunia, na Tanzania ipo tayari kutekeleza mpango huo kwa vitendo ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kulinda maisha ya wananchi na mazingira.

Akizungumza leo Julai 4, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea magari mawili yatakayotumika kwenye kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia chini ya kampeni ya Okoa Maisha na Mazingira, Dk. Kazungu alisema serikali iko mstari wa mbele kuifikia jamii yote kwa elimu ya matumizi bora ya nishati hiyo mbadala.

“Tunashukuru Umoja wa Ulaya na UNCDF kupitia mfuko wa CookFund kwa kusaidia kufanikisha utekelezaji wa mradi huu. Umechangia kubadili maisha na mtazamo wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia,” alisema Dk. Kazungu.

Kampeni hiyo inatekelezwa nchi nzima kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Nishati na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF).

Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau, alisema Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na serikali katika kufanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, huku akibainisha kuwa EU tayari imechangia Euro milioni 19.4 (sawa na Sh. bilioni 59) kutekeleza miradi ya nishati safi katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Pwani, Morogoro na Mwanza.

Balozi Grau aliongeza kuwa magari hayo mawili, yenye thamani ya Euro 130,000, yataleta nguvu katika utoaji wa elimu vijijini, na akaitaka Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo ya vijijini wanapewa kipaumbele katika kupata taarifa na huduma za nishati safi.

“Tunahitaji kuona elimu hii inafika kwa kila Mtanzania, hasa wale walioko pembezoni ambao mara nyingi hutegemea kuni na mkaa kwa kupikia,” alisisitiza Balozi Grau.

Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, chini ya Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano, ili kuhakikisha elimu ya matumizi ya nishati safi inawafikia wananchi wote. Lengo ni kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Mpango huu unalenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda afya za wananchi, kupunguza hewa ukaa na kuhifadhi mazingira, sambamba na kuchochea ajira na maendeleo ya teknolojia za nishati jadidifu nchini.