CHAMA cha Ushirika cha Wafugaji Kiluvya (CHAWAKIM), kimeiomba serikali kusimamia sera inayolinda sekta ya maziwa nchini, ili kuzuia uuzaji holela wa bidhaa hiyo na kuhatarisha afya za walaji
Nicholas Kelya, Mhasibu wa Chama hicho, akizungumza na Nipashe Digital, kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF), amesema kutokana na mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo, mara kadhaa kumekuwapo uuzaji holela hususani kipindi cha masikia.
Amesema msimu wa masika ambao unakuwa na maziwa ya mengi kutokana na uwapo wa malisho kama vile majani, hufanya bidhaa hiyo kuzalishwa kwa wingi na kuuzwa kuholeala ingawa ubora hauzingatiwi kwa baadhi ya wafugaji.
“Maziwa yakiwa mengi msimu wa masika ni rahisi kupatikana kiholela yakiwa hayana ubora. Watanzania wengi hawajali ubora, bali bei. Ukija Ubungo mfano msimu wa masika utakuta mtu analeta maziwa lakini hayana ubora kwa Bei ya Sh. 1,000 kwa lita.
“Bodi ya Maziwa inaweza kutusaidia kusimamia soko kuhakikisha hakuna uuzaji wa bidhaa hii kiholela. Msimu wa masika ambao wanauza na hawajasajiliwa, maziwa sio bora. Chama chetu kama msimu wa kiangazi uliuza lita 14,000 kwa siku, masika utauza lita 10,000.
“Hii ni kwa sababu masika maziwa yako mengi, lakini ubora Je? Hapa tunasisitiza usimamaizi wa sera na utekelezaji,” amesema Kelya.
Pia amesema biashara hiyo inahitaji umakini ili muuzaji asipate hasara, na kwamba bidhaa hiyo inahitajika zaidi katika soko la Dar es Salaam na huku akibainisha kuwa mpango wao ni kujenga kiwanda pamoja na kuanza usamabazaji kwenye shule na kwamba tayari wameanza mazungumzo ya kusambaza bidhaa hiyo shuleni.
“Tunasubiri mchakato wa fedha ukamilike ili tujenge kiwanda, awali walipoanza chama hiki ilikuwa wanauzia chini ya mti hadi wakafikia kuhifadhi lita 800 na sasa tuna uwezo wa kuhifadhi lita 20,500, kwa hiyo tunahitaji eneo rasmi la biashara hii, tuzalishe kitu kikubwa,” amesema.
Amesema chama hicho kina vituo na mawakala kadhaa vya uuzaji Dar es Salaam, huku ubora ikizingatiwa kwanza kubaini iwapo maziwa yamewekwa maji, yamekatika, yametoka kwenye ng’ombe aliyetumia dawa.
“Kwa siku tunakusanya takribani lita 12,000 ya maziwa na kati ya hayo asilimia 40 ni kwa ajili mtindi, ila tunaagiza pia na mkoani Mbeya,” amesema Kelya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED