TEA kuanza na awamu nyingine mafunzo ya kuendeleza ujuzi

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 09:05 PM Jul 04 2025
TEA kuanza na awamu nyingine mafunzo ya kuendeleza ujuzi
Picha:Mpigapicha Wetu
TEA kuanza na awamu nyingine mafunzo ya kuendeleza ujuzi

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), imesema mwaka huu wa fedha itaanza utekelezaji wa awamu nyingine ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ambapo unatarajiwa kutumia Dola za Marekani milioni 30 ndani ya miaka mitano.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam  Salaam na Afisa Uhusiano wa TEA, Eliafile Solla wakati akizungumza na gazeti hili kwenye maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema kwenye mafunzo hayo yatakayoshirikisha vijana wenye umri wa kati pekee jumla ya watu 160, 000 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo .

Amesema awali kwenye utekelezaji wa mafunzo kupitia SDF ulioanza mwaka 2017 na kumalizika mwaka wa fedha 2022/23 lengo lilikuwa kuwafikia watu 35,000 lakini wakati wa utekelezaji mahitaji yalikuwa makubwa na mpaka unakamilika mwaka jana wanufaika walikuwa 49,000.

Amesema baada ya mafunzo kukamilika mamlaka ya elimu ilifanya tathmini (tracer study), kutaka kubaini namna wanufaika wa mafunzo hayo wanavyoanzisha biashara zao na shughuli mbalimbali kutokana na mafunzo waliyoyapata.

Amesema kwenye tahmini hiyo  walibaini kuwa asilimia 80 ya wanufaika wote walimudu kujiajiri na wengine kuajiriwa na asilimia 20 tu walikuwa hawajapaweza kuanzisha biashara kutokana na changamoto walizopata.

Amesema kwenye awamu ya kwanza walikuwa wakichukua watu wa rika zote lakini kwenye utekelezaji unaoanza mwaka huu wa fedha watajikita kwa vijana pekee ambao wameshindwa kuendelea na masomo.

“Tutaangalia vijana ambao mfumo rasmi wa elimu haujawatambua, kuna ambao hawajasoma elimu ya msingi, kuna waliosoma wakashindwa kuendelea, wako mtaani hawana cha kufanya kwa hiyo tunaanza awamu nyingine kuwawezesha kwa mafunzo,” amesema

Amesema kwenye maonyesho ya sabasaba TEA imekuwa ikiwaelimisha wananchi kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo ambayo moja ni kutafuta fedha za kusaidia kuendeleza miundombinu ya elimu kwenye shule na vyuo.

“Tumeamua kushiriki maonyesho haya kwasababu tunaamini hapa kuna wadau wetu wengi wa elimu na tutapata fursa ya kuwaeleza huduma ambazo tunazotoa na nyingine ambazo hawazifahamu,” amesema

“Mtu anayechangia mfuko wa elimu ana vitu ananufaika navyo kama kutangazwa kuwa mmoja wa wadau muhimu wa elimu nchini, TEA inawaingiza kwenye kanzidata yake kama wachangiaji wa elimu na wanapewa cheti cha utambuzi kilichosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA na Kamshna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” amesema

Amesema maonyesho yanakusanyika watu wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi na mashirika na kampuni kutoka ndani nan je ya nchi kwa hiyo ni fursa kubwa kwao kuelezea huduma zinazotolewa.

“Watu wengi waliokuja kwenye banda letu wameelezea kufurahishwa na huduma zetu na wameonyesha utayari wa kufanyakazi na TEA na kutoa fedha zitakazotumika kujenga miundombinu ya elimu,” amesema