TUME ya Ushindani (FCC) imesema mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali yamesaidia kuvutia wawekezaji wengi na kuchangia ufanyaji biashara nchini kuimarika zaidi
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa akizungumza baada ya kutembelea Banda la Tume hiyo katika maonesho ya 49 ya kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya sabasaba, amesema mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, yamesaidia kulinda na kuimarisha sekta ya biashara.
Khadija amesema sheria zinazosimamia biashara na uwekezaji Tanzania ni imara, na bora na madhubuti.
"Lengo la kuanzishwa kwa Tume ya Ushindani (FCC) ni kusimamia na kuimarisha ufanyaji wa biashara nchini, kulinda walaji dhidi ya mienendo isiyofaa ya hali ya ufanyaji biashara kati ya kampuni na kampuni,pamoja na kudhibiti bidhaa bandia."amesema Ngasongwa
"Tunataka kuhakikisha kwamba wawekezaji ndani ya nchi wanatambua kuwa kuna sheria madhubuti ambazo zitawalinda na kusimamia uwekezaji wao wanaoufanya."
Ngasongwa amesema FCC itaendelea kutimiza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Akizungumzia kuhusu maonesho ya 49 kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya sabasaba, Ngasongwa amesema ushiriki wao katika maonesho hayo ni fahari kubwa,huku akiwaomba wageni wanaopita kwenye maonyesho8 hayo kuchangamkia fursa za uwekezaji
Akizungumzia suala la mwekezaji mwenye mtaji mdogo, Ngasongwa amesema mfanyabiashara wa aina hiyo anaweza kupata fursa kuungana na mwekezaji mwenye kipato kikubwa au mwenye uwekezaji mkubwa na kuendesha shughuli zao pamoja.
FCC ni miongoni mwa taasisi ambazo zimekuwa zikishiriki kila mwaka katika maonesho hayo ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ikivutia idadi kubwa ya watembeleaji wanaokwenda kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na tume hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED