NaCoNGO walia changaamoto ufadhili, kukutana Dodoma

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 08:16 PM Jul 04 2025
Jasper Makala (katikati) akizungumza jijini Dar es Salaam leo.
Picha: Sabato Kasika
Jasper Makala (katikati) akizungumza jijini Dar es Salaam leo.

Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini, yamesema kusitishwa kwa ufadhili kutoka nje kumesababisha mengi kuyumba na kushindwa kujiendesha kikamilifu.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam leo na mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Taifa (NaCoNGO), Jasper Makala. 

Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumzia maandalizi ya kongamano la tathmini ya miaka mitano ya mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya taifa, mafanikio, changaamoto, fursa na matarajio.

"Tunatarajia kufanya kongamano kuanzia Agosti 11 hadi 13 mwaka huu jijini Dodoma, lakini ukosefu wa ufadhili kutoka nje unakwamisha mashirika mengi," amesema Makala.

Amefafanua mashirika mengi yamesajaliwa kwa ufadhili toka nje, na kwamba USAID ni mmoja wa wafadhili lakini ufadhili wake umesitiahwa na kusababisha changaamoto kwa baadhi ya mashirika kujiendesha.

"Lakini bahati nzuri serikali ililiona hilo na kuagiza kutengeneza mkakati endelevu wa mashirika haya Kwa mbinu mbalimbali za kujiendesha, tutapata muda wa kutosha wa kujadiliana kuhusu mikakati ya kuendeleza mashirika yetu," amesema.

Vickness Mayao (kulia), akizungumza jijini Dar es Salaam.
Msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali, Vickness Mayao, amesema Tanzania ina mashirika 10,990 ambayo yamekuwa yakifanya shughuli mbalimbali ndani ya jamii.

"Lakini mengine hukwama kujiendesha kutokana na kukosa ufadhili na kujikuta yakionekana kama hayapo na kumbe ni kukosa fedha za kuendeshea miradi," amesema Vickness.

Amesema shirika kutofanya kazi kwa mwaka mmoja au miwili, haina maana kwamba limeahindwa kujiendesha au ni la mfukoni Bali mengine huandika miradi na kuomba fedha kwa wafadhili na kukosa.

"Mashirika yanayokumbana na changaamoto hiyo huwa tunayapa nafasi ya kujipanga zaidi ili yakipata fedha za ufadhili yaweze kufanya ambayo yamekusudia kuifanya ndani ya jamii," amesema.