Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Kampuni ya SICPA Tanzania, inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mchango wa teknolojia katika kulinda walaji, kuimarisha ulipaji wa kodi, na kulinda uchumi wa Taifa.
Jitihada hizo ni sehemu ya mkakati wa TRA wa kuendeleza uwazi, uwajibikaji, na kuujenga uchumi shirikishi unaowanufaisha Watanzania wote.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja wa Mradi wa ETS kutoka TRA,Abyud Tweve alisema
Biashara haramu zinavuruga ushindani wa haki na kupunguza mapato ya serikali, jambo ambalo linaathiri utoaji wa huduma za msingi kama afya, elimu na miundombinu.
Alisema kuwa kwa kutambua changamoto hizo, TRA imeongeza nguvu katika kutoa elimu kwa wananchi, ikiwemo ushiriki wake kwenye majukwaa muhimu ya kitaifa na kimataifa kama vile Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ili kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwaonyesha namna mifumo ya kisasa ya kodi inavyowanufaisha.
"Katika mazingira ya sasa ambapo soko linabadilika kwa kasi, Watanzania wanakumbwa na changamoto nyingi ikiwemo uwepo wa bidhaa bandia na biashara haramu zinazohatarisha afya na usalama wa walaji". alisema
Aliongeza kuwa njia ambazo wananchi watanufaika kupitia elimu hizo ni kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu namna Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) unavyosaidia kutambua bidhaa halali na kulinda walaji dhidi ya bidhaa hatarishi.
"Njia nyinine ni kujifunza kutumia programu ya Hakiki Stempu, ambayo huwasaidia walaji kuthibitisha uhalali wa bidhaa kabla ya kuzinunua. Programu hii rahisi na rafiki kwa watumiaji wa simu janja inawawezesha wananchi kuhakikisha bidhaa kama vile vinywaji baridi, vileo, na sigara ni halali na salama kwa matumizi". alisema na kuongeza kuwa;
"Kuelewa zaidi kuhusu uhusiano kati ya ulipaji kodi na maendeleo ya Taifa, kwa kuelewa kuwa bidhaa halali na kodi inayolipwa huchangia ujenzi wa shule, hospitali, barabara, na huduma nyingine muhimu". alisema
Tweve alisema kuwa teknolojia hizo hazijalengwa tu kwa ajili ya kuimarisha ulipaji wa kodi, bali pia kwa ajili ya kuwalinda na kuwawezesha wananchi.
“Teknolojia hizo hazijaletwa tu kwa ajili ya kuboresha ulipaji wa kodi, bali pia kwa ajili ya kuwawezesha na kulinda afya ya wananchi. Kushiriki kwenye matukio ya kitaifa kama Sabasaba kunatupa nafasi muhimu ya kuzungumza moja kwa moja na wananchi na kuwaonyesha jinsi wanavyoweza kushiriki katika kulinda biashara za haki na kusaidia maendeleo ya Taifa,” alisema Tweve.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa SICPA Tanzania, Alfred Mapunda, alisisitiza kuwa teknolojia inapoambatana na uelewa wa jamii, huwa ni nguvu kubwa ya kuleta maendeleo.
“Teknolojia inapoambatana na uelewa wa jamii inakuwa nguvu kubwa ya kuleta maendeleo. Ushirikiano wetu na TRA unaonyesha dhamira ya kuhakikisha kila Mtanzania anaelewa na kutumia teknolojia hizi kulinda haki zao, kusaidia uwazi, na kujenga soko lenye usawa,” alisema Mapunda.
Ushiriki wa TRA katika majukwaa kama Sabasaba unaonyesha nia ya dhati ya mamlaka hiyo kufanya kazi kwa ukaribu na wananchi, kujenga utamaduni wa ulipaji kodi, na kukuza uwajibikaji wa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
TRA inawahimiza Watanzania wote kuikumbatia teknolojia hiyo, kuendelea kujielimisha, na kushiriki kikamilifu katika kulinda maslahi yao binafsi na ya kitaifa, ili kuimarisha uchumi wa nchi kwa njia endelevu na shirikishi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED