CCM ndio inasababisha umaskini wa watu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:56 PM Jul 04 2025
Makamu Mwenyekiti Bara wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita.

Makamu Mwenyekiti Bara wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, ameikosoa vikali serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kile alichokieleza kuwa ni kushindwa kwao kuwahudumia wananchi na kuwaacha wakiteseka katika umasikini wa kutupwa.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Julai 3, 2025 katika Jimbo la Muhambwe, Mkoa wa Kigoma, Mchinjita alisema kuwa raia wengi wamekuwa wakifariki katika hospitali za umma kwa kukosa dawa, huku wale wanaofiwa wakishindwa kupewa miili ya wapendwa wao hadi walipie gharama.

“CCM imewageuza raia wa nchi hii kuwa maskini wa kutupwa. Wanakufa hospitalini kwa kukosa dawa. Ndugu yako anapofariki, hupewi maiti hadi ulipie,” alisema Mchinjita mbele ya umati wa wananchi.

Mchinjita alisisitiza kuwa hali hiyo ni kielelezo cha serikali iliyoshindwa kuweka kipaumbele katika maisha ya Watanzania, na akawahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao ili kuleta mabadiliko ya kweli kupitia ACT Wazalendo.

Hotuba hiyo ni sehemu ya ziara ya viongozi wa ACT Wazalendo mkoani Kigoma, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.