Mahakama ya Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera, imemhukumu Afisa Mifugo wa Kata ya Kanyigo, Eliezer Leonard Babu (35) kutumikia kifungo cha mwaka mmoja na mwezi mmoja jela kwa makosa mawili ya rushwa, ikiwemo kujipatia manufaa binafsi na kutowasilisha kiasi cha Sh milioni 2.58 za makusanyo ya tozo za Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Yohana Muyombo, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha makosa hayo pasipo kuacha shaka yoyote.
Hakimu Muyombo alisema mahakama imeamua kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na kwa wafanyakazi wengine wenye tabia ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa ukiongozwa na mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera, Kelvin Murusuri na Sospeter Joseph.
Mawakili hao waliwasilisha mashahidi sita na vielelezo nane, ambavyo vilithibitisha bila shaka kwamba mshtakiwa alihusika na makosa hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED