WAKAZI 2,745 wa vitongoji vinne vya kijiji cha Mwadui, Kata ya Nyankende, Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, vimepata huduma ya maji safi na salama.
Hatua hiyo inasaidia kuondokana na matumizi ya maji machafu yaliyokuwa yakisababisha watu kupata magonjwa ya kuhara na kuumwa matumbo.
Pia huduma hiyo, imewaondolea adha wanafunzi wa shule ya msingi Sinwankele, kutumia muda mwingi kutafuta maji ya matumizi ya msalani.
Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kahama, Mhandisi Paschal Mnyeti, ameyabainisha haya wakati wa uzinduzi wa upanuzi wa skimu ya maji Nyankende kwenda kijiji cha Mwadui, utakaohudumia vitongoji vinne vya Ilyamchele, Mwadui A, Igalula na Sinwankele.
“Watoto wetu walikuwa wanarudi kutoka shule wakiwa wamechoka sana na nikwasababu ya kutafuta maji, sasa hali hii wameondokana nayo baada ya kufikiwa na mradi wa majisafi na salama shuleni na wanasoma vema na imetuondoa hofu yao kutokufanya vema kwenye masomo,” ameongeza Antony.
Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, amesema serikali kupitia Wizara ya Maji, imeendelea kutatua changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama katika maeneo ya pembezoni na kuwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na miradi yake, ili iendelee kuwanufaisha vizazi vyote.
Pia amesema, hivi karibuni walisaini mkataba wa upelekaji wa maji ya Ziwa Victoria kutoka Kahama-Ushetu, wenye gharama ya Sh. bilioni 44 na awamu ya kwanza utawafikia wananchi wa kata 11 na umetoa fursa za ajira zisizohitaji ujuzi kwa vijana wa kata husika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED