Wadau kutoka sekta mbalimbali wamekutana kujadili mbinu bora za ushirikiano kwa usimamizi endelevu wa rasilimali maji ndani ya maeneo ya kiuchumi. Mkutano huo umejikita katika mbinu za uvumbuzi, ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma, matumizi ya teknolojia, na sera endelevu ili kuhakikisha matumizi bora na uhifadhi wa rasilimali maji kwa maendeleo jumuishi.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na njia bora za kutumia tena maji yaliyotumika viwandani kwa njia salama, bila kuathiri vyanzo vingine vya maji.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji wa Sekta Binafsi, Aristides Robert Mbwasi, alisisitiza kuwa ni jukumu la kila mmoja kulinda vyanzo vya maji ili kuendeleza viwanda bila kuathiri jamii.
"Hapa tunaangalia namna salama ya matumizi ya maji yaliyotumika viwandani ili yasiathiri watumiaji wengine kama vile wakazi wanaotegemea mito na mabwawa," amesema Mbwasi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmassy, ameeleza kuwa mkutano huo, uliowakutanisha washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya, unalenga kujengeana uwezo na kushirikiana katika changamoto za uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Akitolea mfano Jiji la Dar es Salaam, Mmassy amesema kuwa mito imekuwa ikitumika kama sehemu ya kutupia taka, hali inayosababisha maradhi na kuharibu vyanzo vya maji.
"Asilimia 70 hadi 80 ya viwanda vya Dar es Salaam vinatumia maji ya Mto Ruvu, hivyo utupaji wa maji taka unaharibu hazina ya maji ardhini. Tunatafuta njia za kiteknolojia kuhakikisha maji yanayotumika viwandani yanaweza kurudi katika mzunguko wa matumizi kwa njia salama," amesema.
Mkutano huo wa siku tatu unaofanyika jijini Dar es Salaam umewakutanisha washiriki kutoka nchi zinazotekeleza mpango wa GIZ NatuReS, zikiwemo Tanzania, Ethiopia, Zambia, na Afrika Kusini.
"Tunalinda maji, lazima yahifadhiwe!"
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED