FAMILIA ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chonchorio anayedaiwa kutoweka Jumapili asubuhi akiwa kwenye mazoezi, eneo la Nyakato jijini Mwanza, imejitokeza hadharani kuwasilisha kilio chao kuomba msaada kwa umma.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Machi 25, 2025, dada wa kada huyo, Lucy Mrimi, amesema familia iko katika sintofahamu na kila kitu kimesimama kutokana na kupotelewa na ndugu yao katika mazingira ya kutatanisha.
Amesema kada huyo ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Taifa alitoweka Jumapili iliyopita Machi 23, 2025 majira ya saa mbili asubuhi, alipokuwa anaenda kwenye mazoezi.
"Tunaamini vyombo vyetu vya usalama vinaweza kumpata ndugu yetu na kuwapata wahalifu waliotenda ukatili huu. Tunawaomba Watanzania wote na kipekee Rais wetu Samia Suluhu Hassan, atusaidie tuweze kumpata kaka na nguzo yetu ya familia,” amesema.
Chonchorio ambaye pia ni mfanyabiashara, mkazi wa Nyakato jijini Mwanza anadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha Jumapili asubuhi.
Mbali ya biashara, hivi karibuni kada huyo alitangaza nia ya kugombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Tarime Mjini katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Jana Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP Audax Majaliwa, alithibitisha kupata taarifa za kupotea kwa kada huyo na kueleza kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu kutoweka kwake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED