Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kupitia Mkoa wa Kikodi Kagera, imeendesha operesheni kubwa ya kudhibiti ukwepaji wa kodi kwa njia ya uzalishaji wa pombe kali kinyume cha sheria. Katika operesheni hiyo, TRA ilikamata jumla ya chupa 25,433 zenye ujazo wa mililita 100, 125, na 200 ambazo zilikuwa zinauzwa bila usajili, leseni, au stempu za kodi za kielektroniki (ETS).
Zoezi hilo lilifanywa na Ofisi ya TRA Mkoa wa Kagera ikiongozwa na Meneja wa Mkoa, Castro John, kwa kushirikiana na Meneja wa Wilaya ya Karagwe, William Mneney. Kufuatia operesheni hiyo, watuhumiwa wa ukwepaji wa kodi ambao ni Mwesiga Reopard Rupia, Nelius Kaizelege Mwami, Julieth Ishengoma Kisheni, na Mlokozi Egibert Emely wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba jana Machi 24, 2025 wakikabiliwa na mashtaka ya ukiukwaji wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa (Usimamizi wa Viwango).
TRA imetoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini kuhakikisha wanazingatia sheria kwa kutumia Stempu za Kielektroniki za Kodi (ETS) ili kuepuka hatua kali za kisheria.
Matumizi ya stempu bandia yamekuwa yakichochea biashara haramu ya bidhaa, hali inayoweza kuhatarisha afya ya walaji, kuleta ushindani usio wa haki kwa wafanyabiashara waaminifu, na kusababisha upotevu mkubwa wa mapato ya kodi. Kwa mujibu wa TRA, biashara haramu ya pombe pekee inasababisha upotevu wa mapato ya takriban TZS trilioni 1.2 kwa mwaka kutokana na kodi ya ushuru inayopotea.
Serikali imechukua hatua kali kukabiliana na biashara haramu kwa:
✅ Kuanzisha timu maalum za ukaguzi wa bidhaa zinazotozwa ushuru kwa kutumia vifaa vya kuthibitisha stempu za ETS.
✅ Kuajiri wafanyakazi wapya 1,000 wa TRA ili kudhibiti magendo ya bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa kutoka nje.
✅ Kuanzisha mfumo wa ETS mwaka 2019 ili kufuatilia bidhaa zinazotozwa ushuru kutoka uzalishaji hadi mauzo kwa wateja.
✅ Kutekeleza Aplikesheni ya Hakiki, inayowawezesha watumiaji kuthibitisha uhalisia wa bidhaa wanazonunua.
Stempu za Kielektroniki za Kodi (ETS) zinajumuisha vipengele vya kiusalama vya nyenzo na kidijitali, hivyo kuzifanya kuwa ngumu kughushiwa au kudukuliwa. Stempu hizi hutoa ushahidi wa moja kwa moja unaotumika kuwashtaki wahalifu wa ukwepaji wa kodi.
Katika mazingira ya sasa ambapo biashara haramu inaongezeka duniani kote, Tanzania inasisitiza kuwa udhibiti wa uhakika wa soko ni muhimu, hasa katika kanda ya Afrika Mashariki. Kupitia utekelezaji wa sheria na mfumo wa ETS, TRA inaendelea kuhakikisha uwazi, uzingatiaji wa kodi, na kulinda wafanyabiashara halali kwa ajili ya maendeleo endelevu ya uchumi wa taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED