WAKATI mkataba wa miaka mitano wa beki wa kulia wa Liverpool Trent Alexander-Arnold ukikamilika, timu ya Real Madrid inatajwa kuwa katika hatua za mwisho za uhamisho wa bila malipo wa beki huyo anayekipiga katika Ligi Kuu ya Uingereza.
Real Madrid wanakaribia kukamilisha dili la kumsajili Trent Alexander-Arnold kwa uhamisho wa bure msimu huu wa joto. Beki huyo wa kulia wa Liverpool amekuwa akilengwa na mabingwa hao wa Ulaya na sasa kuna matarajio makubwa kwamba atajiunga na kikosi cha Carlo Ancelotti mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.
Uhamisho huo bado haujakamilishwa na makubaliano yatahitajika kuwasilishwa kwa Liverpool pindi yatakapokuwa tayari.
Vyanzo vya habari nchini Uhispania vimeeleza kuwa Madrid wameweka mezani mkataba wa miaka mitano kwa Alexander-Arnold, na kumtengenezea njia ya ukomo wa uhusiano wake na klabu yake ya utotoni.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 amekuwa muhimu katika mafanikio ya hivi karibuni ya Liverpool na amekuwa bora zaidi msimu huu.
Dhamira ya Madrid kumpata Alexander-Arnold, ambaye ameichezea Liverpool mechi 349 tangu alipocheza kwa mara ya kwanza mwaka 2016, ambako ombi lao lilikataliwa mwishoni mwa Desemba.
Liverpool, ambao wanakaribia kutwaa taji lao la kwanza la EPL tangu 2020, hawakuwa na nia ya kumuuza Alexander-Arnold katikati ya kampeni ya kwanza ya Arne Slot kuwa mkufunzi. Lakini hawajaweza kukubaliana mkataba mpya na mchezaji huyo na amekuwa huru kuzungumza na vilabu vingine kuhusu makubaliano ya awali ya kandarasi tangu mwanzoni mwa mwaka.
Alexander-Arnold ataungana na rafiki na mchezaji mwenzake wa Uingereza, Jude Bellingham klabuni hapo ambako Madrid wana historia ya kusajili wachezaji wakuu kutoka Uingereza wakiongozwa na David Beckham katika historia akifuatiwa na Steve McManaman, Michael Owen na Jonathan Woodgate waliokiwasha klabuni hapo wakitokea Uingereza.
Miamba hao wa Uhispania pia wamekuwa na mazoea ya kunyakua talanta bora zaidi barani Ulaya kwa uhamisho wa bure katika miaka ya hivi karibuni. Wametumia utaratibu huo kuwasajili Kylian Mbappé, David Alaba na Antonio Rüdiger.
Hata hivyo, Liverpool wako hatarini kupoteza wachezaji wake watatu muhimu kwa uhamisho wa bure. Ambao ni Virgil van Dijk na Mohamed Salah ambao pia mkataba wao umeisha na hali zao bado hazijatatuliwa. Van Dijk, beki wa kati wa Uholanzi, amesema "hajui" kuhusu mustakabali wake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED