TAKUKURU yashauriwa kumulika mamlaka za uteuzi wagombea uchaguzi mkuu

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 01:10 PM Mar 26 2025
TAKUKURU yashauriwa kumulika mamlaka za uteuzi wagombea uchaguzi mkuu.
Picha: Mpigapicha Wetu
TAKUKURU yashauriwa kumulika mamlaka za uteuzi wagombea uchaguzi mkuu.

Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga imeshauriwa kuweka watu watakaosaidia kukemea vitendo vya rushwa katika mamlaka za uteuzi wa nafasi za wagombea ili kupunguza vitendo hivyo.

Hayo yamesemwa na wajumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Tanga wakati wa mafunzo ya viongozi wa dini kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2025, yaliyoandaliwa na TAKUKURU mkoani humo.

Walisema katika mamlaka hizo mara nyingi kuna utata wa majina ya wagombea yanayoteuliwa hayawaridhishi wananchi, kwani mengi yanakuwa siyo machaguo yao, kitendo ambacho kimetafsiriwa kuwa ni utoaji wa rushwa wa wagombea hao ambao wengi wao hawana uwezo wa kuongoza.

"Simamieni kwa ujasiri bila woga kutangaza jina la mgombea anayestahili kuwa kiongozi bora atakayewahudumia wananchi lakini siyo kwa maagizo kutoka kwa mtu mmoja kwa matakwa yake ili kutimiza lengo lake," alisema Emmanuel Mkai, mjumbe.

1

"Lakini pia TAKUKURU iweke watu wao katika maeneo ya kutolea huduma za kijamii ambao watakuwa wakikemea moja kwa moja utoaji na upokeaji wa rushwa, hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo hivi," aliongeza Mkai.

Mafunzo hayo yalilenga kuhamasisha viongozi wa dini na jamii kwa ujumla katika kupambana na vitendo vya rushwa, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, na kuhakikisha kuwa viongozi bora na waadilifu wanachaguliwa.