MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira amesema nchi inakopa kwa ajili ya kufanya mambo ambayo yatadumu kwa muda mrefu na kunufaisha wananchi kwa kizazi cha sasa na baadae.
Amesema deni lililoko sasa la Sh. trilioni 97 sio kwamba lote limekopwa na Rais Samia Suluhu Hassan bali limekuwepo tangu enzi za Rais wa kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Wasira ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wanachama pamoja na viongozi wa CCM Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu katika kikao cha ndani kikiwa sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kukagua uhai wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusikiliza kero za wananchi.
“Tunakopa ili kufanya jambo ambalo tutaishi nalo na faida zake kwa miaka mingi kizazi hiki na hata kizazi kijacho na lile deni sio kwamba amekopa Rais Samia trilioni 97 sio kweli," amesema na kuongeza;
"Lile deni linaongezeka na madeni mengine ya zamani ambayo tulishakopa tangu enzi za Nyerere, alichukua miaka 40 kuanza kulipa nayo yamo katika hesabu," amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED