BEI ya nyama imepanda kutoka 9,000 hadi 13,000 kwa kilo moja, hali inayowafanya wananchi wengi kushindwa kumudu kitoweo hicho.
Wakuzungumza kwa nyakati tofauti, wananchi waliofika kununua kitoweo hicho, kwa ajili ya Sikukuu ya Eid, wamesema mabadiliko ya bei yamekuwa ghafla sana.
“Tumetoka kwenye mfungo wa Ramadhani ambako vyakula vilipanda sana bei na sasa tunasherehekea tunakutana na bei ya nyama imepaa ghafla, hii inatuumiza sana,” amesema.
Mwandishi ametembelea eneo la Tegeta, Kiluvya Madukani, Kinondoni, Tabata ambako kote bei ya nyama ilikuwa kubwa tofauti na siku mbili zilizopita.
Mfanyabiashara eneo la Tegeta, amesema kuna wakati nyama ilishuka hadi Sh. 8,000 kwa kilo na sasa imepanda na kuwa kati ya Sh. 12,000 hadi 13,000 kwa kilo.
Amesema wakati mwingine wafanyabishara wanapandisha bei ya vitu kama vile kunde,choroko, maharage pamoja na mchele wakiamini mwezi wa Ramadhani na Kwaresma, watu wanakuwa na uhitaji zaidi wa vitu hivyo.
Elisha Mgawa, mfanyabiashara wa nyama, amesema kupaa kwa bei kunategemea na namna alivyonunua jumla na kwamba kwenye Machinjio ya Pugu, Dar es Salaam, imepanda na wakati mwingine wanakwenda kununua Bagamoyo, mkoani Pwani.
"Tunaoumia ni wananchi, tunaiomba serikali ifuatilie bei za bidhaa mbalimbali hasa wakati wa mfungo wa Ramadhani na Kwaresma, wanaoumia ni wananchi wake," amesema Neema Jonson.
Naye, Rose Mgani alisema vyakula vingi vimepanda bei jambo linaloonesha kuwa serikali haina namna ya kudhibiti bei na hivyo wananchi kugeuzwa mtaji na wafanyabiashara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED