Shura ya Maimamu yataka marekebisho ya mifumo kabla ya Uchaguzi Mkuu 2025

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 01:36 PM Apr 01 2025
Katibu Mkuu wa Shura hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Picha: Imani Nathaniel
Katibu Mkuu wa Shura hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda.

Shura ya Maimamu nchini Tanzania imetoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kuitisha tena mkutano na wadau wa vyama vya siasa ili kujadili na kufanya marekebisho ya mifumo ya uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Wito huo umetolewa jana, Machi 31, 2025, na Katibu Mkuu wa Shura hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda, alipokuwa akisoma Waraka wa Eid katika baraza la Eid lililoandaliwa na Shura hiyo katika Msikiti wa Tungi, jijini Dar es Salaam.

Sheikh Ponda amesema kuwa haja ya marekebisho hayo inatokana na malalamiko yanayotolewa na vyama vikuu vya upinzani, Chadema Tanzania Bara na ACT Wazalendo Zanzibar, kuhusu mazingira ya uchaguzi nchini.

"Kauli ya CHADEMA ‘No Reform, No Election’ na ile ya ACT Wazalendo ya kupinga uchaguzi wa siku mbili Zanzibar zinaakisi malalamiko ya uchaguzi usio huru na haki, kama ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019, Uchaguzi Mkuu wa 2020, na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024," alisema Sheikh Ponda.

Aliongeza kuwa Shura ya Maimamu imefuatilia kwa karibu kauli mbalimbali kutoka kwa viongozi wa serikali, wanasheria, na viongozi wa dini, ambao kwa nyakati tofauti wamekiri kuwa chaguzi zilizopita zilikuwa na dosari kubwa.

"Mbali na vyama vya siasa, hata baadhi ya viongozi wa serikali, wanasheria, na viongozi wa dini wameeleza kuwa chaguzi hizo zilikuwa na kasoro kubwa kiasi cha kutilia shaka uhalali wake," aliongeza.

Tahadhari kuhusu usalama wa taifa

Sheikh Ponda alionya kuwa kuendelea kwa dosari katika uchaguzi kunaweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi. Shura hiyo imetoa wito kwa Rais Samia kufanya marekebisho ya haraka ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wa 2025 unakuwa huru na wa haki.

"Kwa kuwa mfumo uliopo unaminya haki za kidemokrasia za wananchi, haki ya kuishi, na unahatarisha usalama wa taifa, tunatoa wito kwa Rais Samia kuitisha wadau wa uchaguzi kujadili utekelezaji wa makubaliano ya msingi kuhusu mfumo wa uchaguzi kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025," alisema Sheikh Ponda.

Katika waraka huo, Shura ya Maimamu imeeleza kushangazwa na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kulitaka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2025.

"Tumepokea kwa mshtuko mkubwa tamko la Rais Samia la kuliagiza Jeshi la Ulinzi (JWTZ) kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Mshtuko wetu unatokana na ukweli kwamba uchaguzi ni suala la kiraia, na jeshi halihusiki na masuala ya kiraia," alisema Sheikh Ponda.

Alieleza kuwa ingawa kuna malalamiko kwamba Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wanatuhumiwa kwa kupora haki za wananchi katika chaguzi zilizopita, bado kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, taasisi hizo ndizo zinazopaswa kusimamia usalama wa uchaguzi wa kiraia, si Jeshi la Wananchi.

Shura yataka kufutwa kwa sheria kandamizi

Waraka huo pia umelitaka Bunge la Tanzania kufuta sheria zote kandamizi, hususan Sheria ya Ugaidi, ambayo inatajwa kuwa na athari kwa Waislamu.

"Tunatoa wito kwa Bunge kufuta sheria zote kandamizi zilizotajwa na Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1991. Mojawapo ni Sheria ya Kupambana na Ugaidi, ambayo inamnyima mtuhumiwa haki zake za msingi na mara nyingi hutumiwa kuwatuhumu na kuwakamata Waislamu," alisema Sheikh Ponda.

Alidai kuwa sheria hiyo imesababisha wananchi kuamini kuwa serikali ina ajenda dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Aidha, Shura hiyo ilitaka serikali kuwasilisha ushahidi mahakamani kwa watuhumiwa wa kesi za ugaidi ili waweze kupata haki zao kisheria.

"Ni kinyume na haki za binadamu kuwaweka watu gerezani kwa miaka kadhaa, hata kufikia 10, bila kusikilizwa mahakamani na kuthibitishiwa hatia zao," aliongeza Sheikh Ponda.

Shura ya Maimamu ilisisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali kushughulikia masuala haya kwa haraka ili kuimarisha haki, amani, na utulivu wa taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.