KUSUKA nywele kwa mitindo tofauti kwa watu wenye asili ya kiafrika, ni utamaduni uliodumu kwa karne.
Muundo wa asili wa nywele za mwafrika kutokana na ugumu wake unawezesha kusukwa na kudumu kwa muda mrefu tofauti na jamii zingine kutoka mabara nje ya Afrika.
Shirika lisilo la kiserikali za Marekani liitwalo ‘Consumer Reports’, limefanya majaribio kwa sampuli aina 10 maarufu za nywele bandia na kubaini zote zina kemikali zinazoweza kusababisha saratani.
Matokeo ya utafiti yabainisha kuwapo nywele bandia ambazo pia zina madini ya risasi, zina mgusano wa moja kwa moja na kemikali hizo hatari kwa muda mrefu, zilizosukwa vichwani mwao.
Utafiti huo mpya umeonesha nywele bandia zinazotumiwa na wanawake wengi weusi, yaani waafrika, zinaweza kuwa na madhara kwa afya zao.
Mitindo ya nywele ya kisasa ya kusuka kwa kuongezea nywele zingine bandia, kwa jina maarufu rasta, ni maarufu sana kwa wanawake weusi, ikiendelea kupendwa na watu mashuhuri na kinamama wa koo zao.
James Rogers, Mkuu wa Majaribio ya Usalama wa Bidhaa katika shirika la Consumer Reports, anasema "matokeo haya yanatia hofu kwa sababu wanawake wanakuwa katika mgusano wa moja kwa moja na kemikali hizi hatari kwa muda mrefu wanapokuwa na nywele zao zilizofumwa na kusukwa vichwani mwao.
"Tunaamini kwamba kila unapokutana na kemikali hatari, madhara yake hujilimbikiza na huongezeka baada ya muda."
Hata hivyo, Rogers anasisitiza kuwa utafiti zaidi unahitajika, akisema: "Tunatumaini hii itaanzisha mjadala, si tu katika ngazi ya udhibiti, bali pia ndani ya jamii zetu kuhusu umuhimu wa kupata taarifa sahihi."
Josée na binti zake Abigail na Naomi, ambao wanafanya kazi naye saluni, wameona ongezeko la wateja wapya, hasa baada ya kusaidia kutengeneza nywele za wigi lililotumiwa na mhusika Elphaba katika filamu Wicked, moja ya filamu zenye mapato makubwa zaidi kwa mwaka 2024.
Hata hivyo, baadhi ya wateja wao wameingiwa na wasiwasi. Kwa Kellie-Ann, ambaye anasukwa kwa mara ya kwanza katika saluni ya Josée, anasema ripoti hiyo imemshtua sana.
"Ninaona ni mbaya kwamba kampuni zimekuwa zinatufanyia haya kwa miaka mingi. Tunastahili kilicho bora zaidi," analalama.
Anasema anatafuta chapa za nywele zisizo na kemikali hatari na plastiki.
"Wanawake wengi niliozungumza nao wamekubaliana kuwa nywele zinazoweza kuharibika kiasili ni bora, pia ni nzuri kwa mazingira," anasema.
Kwa upande mwingine, Ifeanyi, ambaye pia amekuwa akisuka nywele zake tangu utotoni, anasema ripoti hiyo haimtishi sana.
Anahoji kuwa watu huweza kukutana na kemikali hatari kila siku kupitia vyakula vilivyosindikwa, pombe na sigara.
"Ni vyema kuwa waangalifu, lakini siamini kwamba tunapaswa kuachana kabisa na mtindo huu wa nywele," anasema.
Ana wasiwasi kuwa mijadala katika mitandao ya kijamii inaweza kuwafanya watu waogope kusukwa, jambo ambalo linaweza kuwa na athari mbaya kwa wafanyabiashara weusi katika sekta ya nywele.
Mwaka 2021, Treasure Tress, kampuni ya urembo ya Uingereza, iligundua kuwa wanawake wa Uingereza wenye ngozi nyeupe (wazungu) walitumia euro milioni 168 kwa bidhaa za nywele kwa mwaka.
Utafiti wa awali za L'Oréal ulionesha kuwa wanawake weusi Uingereza, hutumia mara sita zaidi ya gharama kwa ajili ya nywele zao kulinganishwa na wanawake wengine.
"Ilikuwa bora kuona kampuni ikifanya juhudi kuhakikisha bidhaa zao ni salama kwa watumiaji, badala ya kutufanya tuhisi kuwa baadhi ya tamaduni zetu za asili ni mbaya," alisema Ifeanyi.
Kwa wengine, mabadiliko katika mtazamo kuhusu nywele bandia yanafungua milango kwa biashara mpya.
Tendai Moyo, alianzisha kampuni yake inayouza nywele za asili kutoka Kusini-Mashariki mwa Asia mwaka 2021, ikiuza pia nywele bandia zinazoweza kuharibika kiasili, zilizotengenezwa kwa nyuzi za collagen.
Tangu kuchapishwa kwa utafiti huu, ameona ongezeko kubwa la mahitaji, hasa Marekani.
Lakini anasema hii ni sehemu ya mwelekeo mpana, kwa kuwa tangu janga la UVIKO-19 litokee, watu wengi walijaribu mitindo mipya ya nywele wakiwa nyumbani.
Hata hivyo, moja ya changamoto kubwa ni bei ya bidhaa mbadala. Nywele za kampuni yake zinagharimu mara 2.5 zaidi ya chapa za kawaida zinazopatikana madukani.
Ifeanyi alisema bei hizo si rahisi kwa wanafunzi kama yeye: "Unapotumia fedha kununua nywele hizi, ni sawa na gharama ya kusukwa, kwa hivyo unajikuta unalipa mara mbili."
Tendai alijitetea kwa kulinganisha na vyakula vyenye afya dhidi ya vyakula vyenye afya, akisisitiza kuwa bidhaa zake zinaweza kutumika tena, hivyo kusaidia kupunguza gharama kwa muda mrefu.
Katika saluni ya Josée, Naomi alisisitiza kuwa ususi si kazi tu, bali ni utamaduni unaounganisha familia.
"Nimekuwa ninasuka tangu nilipokuwa na miaka sita," anasema huku mama yake akitabasamu kwa fahari.
"Ni kazi inayotupa nguvu," aliongeza, akisema kuwa ni heshima kufanya kazi inayowawezesha wanawake wengine kujisikia vizuri na wenye kujiamini.
Licha ya hofu inayoongezeka kuhusu athari za kiafya, ususi unabaki kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa wanawake weusi.
Chanzo: BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED