CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), kimetangaza fursa kwa wananchi wenye nia ya kugombea nafasi za udiwani na ubunge, kuchukua fomu bure ndani ya chama hicho.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za chama katika kuhamasisha na kuwapa nafasi wananchi wenye malengo ya kushika nafasi za uongozi, ili kuleta mabadiliko na maendeleo kwa jamii yao.
Akizungumza na Nipashe, leo, Katibu Mwenezi wa Chama hicho, Ipyana Samson alisema chama kimetoa fursa kwa mwananchi yeyote mwenye nia ya kugombea ubunge na udiwani kujiunga na kuchukua fomu bure.
Ipyana amesema wameamua kufanya hivyo, ili kuhakikisha watu wa kila tabaka, bila kujali hali yao ya kiuchumi, wanapata nafasi ya kushiriki katika uchaguzi na kuchaguliwa kama demokrasia inavyotaka.
Ameongeza kuwa mpango wa CHAUMMA ni kusimamisha wagombea katika kila kata na jimbo nchini na kwamba, ili kuyafikia maeneo yote wananchi hususan vijana wanahamasishwa kujitokeza.
“CHAUMMA kinakaribisha mwananchi yeyote kujitokeza kugombea nafasi ya udiwani au ubunge, vijana hii ni fursa kwenu kupata ajira na kutimiza malengo yenu,” amesema Ipyana.
Ameongeza kuwa chama hicho hakitagomea uchaguzi huo, watashiriki kikamilifu na kwamba wanaendelea kukamilisha ilani ya uchaguzi ya chama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED