Watu saba wafariki, 42 wajeruhiwa ajali ya basi Mwanga

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 03:12 PM Apr 03 2025
Watu saba wafariki, 42 wajeruhiwa ajali ya basi Mwanga

Watu saba wamefariki dunia na wengine 42 wamejeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Mvungi lenye namba za usajili T.222 DNL, aina ya Yutong, kupinduka na kutumbukia bondeni katika kijiji cha Mamba Msangeni, wilayani Mwanga, saa 12 asubuhi Aprili 3, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyeshindwa kulimudu gari alipokuwa akijaribu kukwepa gari jingine kwenye kona kali. Basi hilo lilikuwa likitokea Ugweno kuelekea Dar es Salaam.

Majeruhi wa ajali hiyo wanapatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali, zikiwemo Hospitali ya Kifula, Hospitali ya Wilaya ya Mwanga, Hospitali ya KCMC Moshi, na Hospitali ya Mkoa wa Mawenzi.

Majina ya Waliopoteza Maisha

Mamlaka zimethibitisha vifo vya watu saba waliotambuliwa kuwa:

  1. Ashura Omari Sakena (47) – Mkazi wa Vuchama, Mwanga
  2. Zaituni Hashimu Mwanga (52) – Mkazi wa Masumbeni, Mwanga
  3. Shabani Omari (62) – Mkazi wa Mwanga
  4. Judith Saifoi Mwanga (43) – Mkazi wa Mangio, Mwanga
  5. Hadija Omari (2) – Mkazi wa Mwanga
  6. Haji Abubakar (50) – Mkazi wa Kilifi
  7. Hamadi Hassani (64) – Mkazi wa Nagara, Ugweno

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwanga kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Habari zaidi itakujia hapa hapa...