NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga amesema serikali itaendelea kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu hususani katika athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi kama uwepo wa maafa yanayoleta madhara ikiwemo vifo, uharibifu wa miundombinu na athari za kiuchumi.
Aliyasema hayo leo wakati wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa watu wenye ulemavu unaofanyika jijini Berlin, Ujerumani. Ambao ulianza jana, ukiratibiwa na Shirikisho la Kimataifa la Watu Wenye Ulemavu (IDA), serikali ya Ujerumani, na Jordan.
Pia Naibu Waziri Ummy ameeleza namna Tanzania ilivyojipanga kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu yanapewa kipaumbele kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosaidia katika utekelezaji ya masuala yanayowakabili watu hao.
“Tanzania inazingatia ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali ikiwemo elimu, masuala ya mabadiliko ya tabianchi, fursa za uongozi, kiuchumi pamoja na masuala ya kijinsia,” amesema Ummy.
Ameongeza kuwa katika kutambua athari zitokanazo na maafa hususani kwa watu wenye ulemavu, serikali itaendelea kuweka uangalizi mahususi katika shughuli za usimamizi wa maafa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo huku wakitambua athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi dunia.
“Sheria ya Usimamizi wa Maafa Sura 242 imeweka uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwa Jukwa la Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa. Vilevile, Kanuni za Usimamizi wa Maafa za mwaka 2022 zinaelekeza kuzingatia mahitaji yao wakati wa kufanya tathmini ya madhara na mahitaji kwa ajili ya kukabiliana na maafa na kurejesha hali,” amesema Ummy.
Hata hivyo, ameeleza kuwa Tanzania inazingatia mwongozo wa kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu walioathirika na maafa wa mwaka 2022 unaelekeza kuweka kipaumbele kwa tabaka hilo katika kaya zisizo na uwezo au msaada wa ndugu na jamaa.
Vile vile, amesema miongoni mwa malengo ya mkakati wa taifa wa usimamizi wa maafa 2022-27 ni kuimarisha mchangamano wa jinsia, vijana, watu wenye ulemavu katika usimamizi wa maafa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED