Dk. Biteko: Upotevu wa umeme wazidi kuongezeka, tunahitaji mbinu kudhibiti

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:49 AM Apr 10 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
Picha: Nipashe Digital
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema kiwango cha upotevu wa umeme nchini kimeendelea kuongezeka kutoka asilimia 14.57 hadi 14.61, hali inayozidi kuvuka kiwango kinachokubalika kitaalamu ambacho ni asilimia 12.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utendaji wa sekta ndogo ya umeme kwa mwaka 2023/24 iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dk. Biteko alisema ni lazima kuwepo na mbinu mbadala kuhakikisha upotevu huo unadhibitiwa kwa ufanisi.

“Maana yake ni kwamba lazima tutafute njia mbadala ya kuhakikisha upungufu au upotevu wa umeme unaendelea kudhibitiwa. Kiwango kinachokubalika kitaalamu ni asilimia 12, sisi tupo juu ya kiwango,” alisema Dk. Biteko.

Gharama za Umeme Kufanyiwa Tathmini Mpya

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, alisema kuwa mamlaka hiyo inapanga kufanya tathmini ya gharama za huduma ya umeme katika mwaka ujao wa fedha, kutokana na ukweli kwamba bei za umeme hazijarekebishwa tangu mwaka 2016.

Alifafanua kuwa uamuzi wa serikali kuachana na mitambo ya kukodi ambayo ilitumika kipindi cha nyuma, ulisaidia kudhibiti mfumuko wa bei, ambapo mwaka 2011 bei za umeme zilipanda kwa asilimia 40 na mwaka 2013 kwa asilimia 39.

“Hatua hiyo pamoja na uamuzi wa serikali kubadili deni la TANESCO la takribani Shilingi trilioni 2.4 imeisaidia kampuni hiyo kuendelea kuimarika,” alisema Dk. Andilile.

Mikakati ya Uzalishaji Endelevu wa Umeme

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Prof. Mark Mwandosya, alisema miradi mikubwa ya umeme inahitaji muda mrefu kuanzia upembuzi yakinifu hadi utekelezaji wake kukamilika.

Alisisitiza kuwa kukamilika kwa Bwawa la Nyerere ni kichocheo muhimu kwa ustawi wa sekta ya nishati katika miaka ijayo.

“Vinginevyo, tutajikuta baada ya miaka minne au mitano tunarudi kule kule tulikotoka. Nina uhakika kwamba chini ya uongozi wa Dk. Biteko na Rais Samia Suluhu Hassan, jambo hili litakuwa limeangaliwa kwa kina,” alisema Prof. Mwandosya.