Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Benson Bagonza amewataka watanzania kutumia fursa za kidemokrasia kujenga Taifa linalopenda haki na kutetea wanyonge.
Katika salamu zake za Pasaka 2025 alizoziita ni Salaam za Upendo na Ufufuo toka Uaskofuni Lukajange,amesema mwaka huu ni mwaka wa fursa katika Taifa letu,Yesu amefufuka na kutupatia ujasiri.
"Serikali yetu isigeuze kuwa gulio la kuuza na kununua haki za wanyonge.Tunaqlikwa kuwa chachu ya haki iletayo amani katika Taifa.
"Haki inatosha kuleta na kutunza amani.Tuukatae uzushi wa kuimba wimbo wa amani siyotokana na haki,"amesema.
Askofu Bagonza amesema ni muhimu kukumbuka kuwa Yesu Kirsto hakupatikana na kosa lolote, aliteswa na kuuwawa ili kuwafurahisha wenye mamlaka.
"Furaha ya wenye mamlaka inayotokana na mateso ya wasio na hatia ni ya bandia na ya muda mfupi.Furaha ya watawala ilidumu siku tatu.
"Mwenye haki akatoka kaburini.Msamaha wa mfalme wakati wq sikukuu ulikwenda kwa jambazi Baraba.Yesu hakuhitaji msamaha wa Mfalme ili kutoka kaburini.Alifufuka yuko hai hata sasa.Uhai wake ni uhai wa wote wamwaminio,"amesema.
Askofu Bagonza amesema Bwana Yesu aliyefufuka anatuletea sisi sote habari njema. Anasema kwa kuwa yeye yu hai, basi hata sisi tutakuwa hai.
"Baada ya mateso yote aliyoyapata akiwa mikononi mwa wenye mamlaka; akafa na kuzikwa; hatimaye alifufuka. Kwa kuwa sisi ni warithi halali wa kila kitu cha Yesu Kristo; basi tunarithi mateso yake na sasa anatuambia; tunarithi uhai wake baada ya kufufuka,"amesema."Hakufufuka kwa faida yake mwenyewe bali kwa faida yetu sote. Kufufuka kwake kunawakatisha tamaa wote wanaotumia na kutukuza kifo kama njia ya kuzuia mamlaka zao za kidunia zisihojiwe. Kufufuka kwa Yesu kunachochea watu wengi kukipokea kifo kama njia takatifu ya kurejesha haki katika jamii; yaani, dhuluma inasulubiwa na haki inafufuka. Kwa kupigwa kwake, sisi tumepona,"amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED