RAIS mstaafu na Mshauri Mkuu wa Kongamano la Nane la Uongozi Afrika (ALF), Jakaya Kikwete, amesema ingawa Afrika imepiga hatua kubwa katika kukuza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ni muhimu kutafakari kwa uaminifu kuhusu changamoto ambazo bado zinalikabili bara hilo.
Changamoto hizo, ametaja kuwa ni pamoja na umaskini, magonjwa, ukosefu wa usawa, ujinga, mabadiliko ya tabianchi na kutokuja kusoma na kuandika, akisisitiza kuchukuliwa kwa hatua.
Kikwete amesema haya wakati wa Mkutano wa Nane wa Jukwaa la Uongozi la Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi.
Amesema kuwa mageuzi haya yanahitaji uhamasishaji wa rasilimali, utashi thabiti wa kisiasa na kuimarishwa kwa uwajibikaji.
"Jukwaa hili liwe la mageuzi ambalo linabadilisha tamaa kuwa vitendo na kuongoza uongozi na uvumbuzi kaika mabadiliko," amesema Kikwete.
Amesema lengo la jukwaa hilo ni kupitia hali ya utekelezaji wa SDGs katika nchi za Afrika, kubaini changamoto zinazozuia maendeleo, kuhimiza ushirikiano wa kikanda na kuandaa suluhisho kiubunifu.
Kikwete ameeleza kwamba, licha ya malengo ya SDGs kuwa ya kipevu, imeonyesha kwa uhuru kwamba Afrika imepiga hatua kubwa, iko wazi kuwa Afrika inaendelea na mafanikio yake yaliyopatikana kwa jasho ni ya kweli.
"Kadri tunavyosherehekea maendeleo ya ajabu ya Afrika, lazima tukutane uso kwa uso na changamoto ngumu ambazo bado zinatishia kuzuia maendeleo yetu. Wakati tunaekea mwaka 2030 ipo haja ya kuchukua hatua kubwa Zaidi,".
Amesema ni wakati wa mageuzi ya uhamasishaji wa rasilimali bunifu, kujitolea kwa kisiasa, na enzi mpya ya uwajibikaji. Hebu tuinuke na kukabiliana na changamoto hii na kufanya mustakabali wa Afrika kuwa wa wazi.
Rais mstaafu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn Boshe, alieleza kuwa SDGs 17 ni uwakilishi wa matamanio ya pamoja ya Afrika ya bara lililo huru kutoka kwa umaskini na ukosefu wa usawa.
Amesema Afrika ni bara lenye uwezo mkubwa, linakutana na changamoto nyingi, ikiwamo idadi kubwa ya vijana, rasilimali asilia, mabadiliko ya tabianchi, masuala ya utawala, na umaskini.
"Maendeleo yamepatikana katika kupunguza umaskini, ambapo maeneo mengi yameondoa watu kutoka kwenye umaskini wa kina, ingawa maeneo mengine yamepungua. Katika elimu, viwango vya usajili vimeongezeka na katika afya, kumekuwa na maendeleo katika kupambana na vifo vya akinamama, malaria na Ukimwi ingawa hii imeungwa mkono kwa kiasi kikubwa na ufadhili wa wahisani," amesema.
Amebainisha kuwa uwekezaji katika miundombinu, hasa nishati, unaendelea, hata hivyo, amesema safari bado ni ndefu na mabadiliko ya tabianchi yanabaki kuwa changamoto kubwa zaidi kwa Afrika.
"Utawala bado ni changamoto, kwani masuala kama vile mtiririko haramu wa fedha, migogoro, na rushwa yanapoteza rasilimali zinazopaswa kuelekezwa kwenye uwekezaji wa SDGs.
“Kuna pengo kubwa la fedha, ili kufanikisha SDGs na Afrika inapaswa kutafuta vyanzo vingine vya fedha. Kuimarisha taasisi, kukuza uwazi na utawala bora na kupambana na rushwa ni hatua muhimu za kuongeza kasi ya maendeleo," amesema.
Mwakilishi wa zamani wa FAO nchini Ethiopia, Mafa Chipeta, ameeleza kuwa Afrika haiwezi kutegemea tu maamuzi ya wengine, na ni muhimu kuzingatia kile kinachoweza kuhimili Afrika katika siku zijazo hasa kwa kukuza uchumi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED