KATIBU Mkuu Kiongozi Mstaafu wa Tanzania, Balozi Ombeni Sefue, amesema ili nchi za Afrika zifanikishe kutoa elimu bora, kwa kuwa Afrika imekuwa ikiwekeza kiwango kidogo kwenye masuala ya elimu ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea.
Pia amesema nchi hizo za Afrika zinatakiwa kuzingatia uwekezaji endelevu na imara zaidi kwenye elimu, ukumbatiaji wa teknolojia na masuala ya akili mnemba (AI) pamoja na mabadiliko ya sera za elimu.
Balozi Sefue ameyasema hayo mjini Kampala nchini Uganda, wakati akiwasilisha mada kuhusiana na maendeleo endelevu ya kiafrika katika upande wa elimu katika kongamano la 8 la Uongozi wa Afrika (ALF), lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi.
Amesema nchi nyingi za kiafrika zimeweka bure utoaji wa elimu kwenye eneo la ada na gharama nyingine zikitolewa na mzazi hali ambayo kaya maskini hushindwa kumudu kuwapeleka watoto wao kupata elimu.
Balozi Ombeni amesema kuna vizuizi vingi vya kujiunga na elimu kwa nchi za Afrika, ikiwamo uhaba wa shule za msingi, changamoto za masuala ya kitamaduni na kijamii kama vile ndoa za mapema, mimba za utotoni na upendeleo wa kielimu kwa wavulana.
''Ni ukweli nchi nyingi za kiafrika zimewekeza bure utoaji wa elimu ila katika gharama nyingine kama vile sare, madaftari na vingine, mzazi mwenyewe anatakiwa kuwajibika hali inayosababisha kaya maskini kushindwa kumudu hayo na kushindwa kuwapeleka watoto shuleni," amesema.
Balozi Sefue amesema inapozungumziwa suala la elimu bora ni kuondosha mfumo wa zamani wa kielimu na mitaala yake hususan elimu ya juu na kuwa na elimu ya kuzalisha kazi badala ya kuwa watafutaji wa kazi.
Aidha amesema nchi za afrika zinaweza kutoka zilipo sasa na kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kidijitali hivyo kuinua viwango vya elimu kwa afrika kwa kiasi kikubwa.
Awali akifunga jukwaa hilo, Waziri Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbanja amesema wajumbe wa jukwaa wanatakiwa kufanyiwa kazi yote yanayojadiliwa kwa vitendo kwa ajili ya maendeleo.
Amesema ili kufikia hayo yote ni vizuri suala la ulinzi na amani kuendelea kudumisha katika nchi kwani hauwezi kufikiria maendeleo kama nchi yako haina amani.
Aidha, Nabbanja amesisitiza uwekezaji zaidi katika kilimo cha umwagiliaji ili kuzalisha zaidi na kuuza bidhaa nje ya bara la Afrika na kuendelea kukuza uchumi wa nchi zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED