Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko ameagiza Shirika la Umeme nchini(TANESCO) na mamlaka zingine kufuatilia mikataba 33 ya uzalisha na kuuziana umeme ambayo tangu imesainiwa haijawahi kutekelezwa.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko ameagiza Shirika la Umeme nchini(TANESCO) na mamlaka zingine kufuatilia mikataba 33 ya uzalisha na kuuziana umeme ambayo tangu imesainiwa haijawahi kutekelezwa.
Akizindua ripoti ya utendaji wa sekta ndogo ya umeme kwa Mwaka 2023/24 iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), jijini Dodoma, Dk.Biteko alisema mikataba hiyo mingi inayotokana na umeme wa sola ambayo iko miradi 21 na kwamba hiyo ingeweza kuzalisha umeme Megawati 157.
“Tufuatilie tujue kuna tatizo gani? lakini je kuna sababu ya kuendelea na mkataba maana mtu mmekubaliana lakini hakuna kinachoendelea ni kama wakati Fulani niliwaambia TANESCO wana MoU nyingi mara hii ya sola, hii ya upepo, MoU ukisaini maana yake umefunga mlango wa mtu mwingine kuingia.”
“Wale mliosaini MoU hakuna wanachofanya matokeo yake huwezi kushirikisha mtu mwingine umefungiwa, TANESCO ripoti hii iwasaidie tujue wamefikia wapi,”
Aidha, alisema katika ripoti hiyo inaonesha malalamiko 146 yaliyowasilishwa mengi yalikuwa kati ya TANESCO na wateja wake na ikilinganishwa na mwaka uliopita yalikuwa 92.
“Kwa mujibu wa taarifa malalamiko mengi waliyoyaona asilimia 27 kuhusu na ankra na asilimia 15 kuhusu uunganishaji, asilimia 12 ni watu waliolalamikia huduma kwa wateja, kile kituo ambacho napenda kukitembelea mara kwa mara asilimia 12 ya malalamiko yanalalamikia jambo hilo,”alisema.
Vilevile alisema asilimia 12 wanalalamikia kuhusu tarrif wengine wanadhani bei ni kubwa, asilimia nane wamepata shida kutokana na umeme na asilimia tatu ni uharibifu wa mali.
“Hiki ni kiashiria kingine kuwa EWURA ni kioo cha kutuonesha wapi kuna matatizo, na tunatakiwa kusimamia kwa karibu sana tuangalie wingi wa malalamiko yanatokea wapi na kama kuna mengine ya kutoa elimu, twendeni kwa wananchi wajue sababu gani imetokea,”alisema.
Kuhusu ukuaji wa mahitaji ya umeme, Dk.Biteko alisema katika kipindi hiki wametoka kwenye ukuaji umefikia Megawati 1900 na kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja mahitaji ya umeme nchini yameongezeka na sasa yamefikia Megawati 254.
“Taarifa imetupa tahadhari imetuonesha itakapofika mwaka 2035 mahitaji ya umeme nchini yatafika Megawati 8855 na itakapofika mwaka 2030, mahitaji ya juu yatafika Megawati 4878, hivyo ndicho anachosema Prof.Mwandosya,”alisema.
Alisema kama wataridhika wasiwekeze kwenye nishati kutokana na kasi ya ukuaji wa uchumi kutahitajika umeme mwingi zaidi.
“Lazima tuanze kujenga vyanzo vingine sasa, miradi ya Luhuji Nyumakali, miradi ya sola ya Kishapu, miradi ya upepo Singida, Makambako yote hii tuanze kuijenga sasa hivi na tutumie mradi wetu wa Compact tulionao, kama tutapata fedha tuweke ujasiri mkubwa wa kuwekeza kabla hatujarudi hapa kujadili masuala ya mgao na hili litawezekana, taarifa ya EWURA imetuonesha hatari ya kule tunapokwenda tujiandae kuikabili hii hatari,”alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED