Jamhuri: Washtakiwa wanachelewesha kesi kusikilizwa ushahidi

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:05 AM Apr 10 2025
Mhandisi Faustine Malya.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mhandisi Faustine Malya.

Upande wa Jamhuri katika kesi ya tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kughushi inayomkabili Mhandisi Faustine Malya (44) na wenzake watu umeieleza Mahakama kuwa washtakiwa hao wanachelewesha kesi hiyo kusikilizwa ushahidi kwa makusudi.

Imedai kuwa kila kesi itakapofika kwa ajili ya kusikilizwa washtakiwa wanatoa sababu ambazo sio za msingi, Malya taarifa ya daktari inaeleza kwamba afya yake ya akili imetengemaa lakini yeye anadai hawezi kuendelea kwa sababu bado anaumwa.

Washtakiwa wengine ni Emiliani Kimaro (35) Mkazi wa Kibaha, Nelson Jacob (32) Mkazi wa Kimara Mwisho (wahandisi) na muongoza watalii Tumaini Mollel (30) Mkazi wa mkoani Mwanza, Kiseke, ambapo wanatuhumiwa kwa mashtaka nane.

Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali Burton Mayage akisaidiana na Janeth Kimambo mbele ya Hakimu Mkazi Amos Rweikiza wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa shahidi wa kwanza wa Jamhuri.

Wakili Mayege ametoa malalamiko hayo, baada ya washtakiwa hao kupitia mawakili wao Peter Shapa na Pharis Mshana kugoma kuendelea na usikilizwaji kwa madai kuwa bado hawajakaa na wateja wao wakawaeleza kuhusu kesi hiyo.

Mshtakiwa Malya yeye amedai kwamba hawezi kuendelea kusikiliza kesi kwa sababu akili yake inaweza ikafyatuka, bado hajapona afya yake ya akili.

"Siwezi kuendelea na kesi kwa sababu ya hali yangu ya kiafya cheti hiki hapa halisi na nakala ni kweli naendelea vizuri tofauti na awali nilikuwa napiga watu hata hapa kichwa kinaweza kikacheza akili ikatoka,"


"Nilipokuwa gerezani nilikuwa napiga wenzangu hadi nikafungiwa kwenye chumba maalum kwa hiyo mimi na daktari ndiyo tunajua hali ya akili yangu," amedai Malya


Wakili Mayage amedai kwamba anachokifanya Malya ya kuchelewesha kesi kwa sababu tayari ripoti ya daktari inaeleza kuwa afya yake imetengeemaa, amebakiza matibabu ya nje ya kuzungumza na wanasaikolojia.

Akijibu hoja hizo, Wakili Mayage amedai kuwa hazina mashiko za kusababisha kesi iahirishwe kwa sababu walikuwa na muda mrefu wa kutafuta wakili tangu kesi ilipoahirishwa mara ya mwisho Machi 28,2025.


"Kuhusu Malya tathimini yake ya afya ya akili inaendelea kuimarika kwa hiyo hana sababu ya msingi ya kesi hii kuahirishwa. Naomba tuendelee na usikilizwaji ni mara ya tatu shahidi anarudi bila kutoa ushahidi,"amedai Wakili Mayage


Baada ta kusikiliza hoja hizo, Hakimu Rweikiza alitoa amri kwamba Mei 13,2025 washtakiwa wote wawepo na kesi itasikilizwa haitaahirisha tena usikilizwaji tutaendelea na pia amezingatia hoja za upande wa utetezi.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa walijipatia zaidi ya Sh milioni 300 kutoka Shirika la Nyumba la Taifa tawi la Mtwara, Halmashauri ya Jiji la Tanga, Skyline Properties Ltd, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kampuni ya mafuta ya Comel.

Inadaiwa kuwa walijipatia fedha hizo kutoka kwenye miradi inayosimamiwa na Kampuni ya Sec East African Ltd inayohusiana na masuala ya kufunga lifti katika majengo mbalimbali , baada ya kubadilisha akaunti namba za Kampuni hiyo na kuweka namba zao za akaunti za benki.

Ilidaiwa kuwa walifanikiwa kufanya hivyo, baada ya kughushi sahihi ya Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Tian Chun,  Sahihi ya Mkurugenzi wa Masoko Ntuli Mwankusye na sahihi ya Mhasibu Gabriel Makundi.

Washtakiwa hao wanatuhumiwa kutenda makosa hayo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kughushi kati ya Novemba 5,2021 hadi Aprili 14,2023 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.