Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wilayani Kahama wameiomba serikali kuwasaidia kupata huduma ya umeme kwenye migodi yao ili kupunguza gharama kubwa za uendeshaji, kukuza uchumi wao na kuongeza makusanyo ya maduhuri kwa serikali.
Ombi hilo limewasilishwa leo wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, alipotembelea migodi midogo kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji hao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wanawake Tanzania (TAWOMA), Bi. Semeni Malale, amesema kukosekana kwa umeme kumesababisha wachimbaji kutumia majenereta, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji hadi kufikia zaidi ya Shilingi milioni 10 kwa mwezi kwa mafuta pekee—gharama kubwa kulinganisha na mapato wanayopata.
Amesema mgodi wa Nyamishiga, unaosimamia ukusanyaji wa maduhuri ya serikali, umeshuhudia kushuka kwa mapato kutoka Shilingi milioni 70 hadi kati ya milioni 3 hadi 8 kwa mwezi, kutokana na wachimbaji wengi kuhama kwenda maeneo yenye huduma ya umeme na maji.
“Mgodi huu uliwahi kuwa na zaidi ya wachimbaji 3,000, lakini sasa waliobaki hawazidi hata 200 kwa sababu ya kukosekana kwa nishati ya uhakika,” alisema Malale.
Kwa upande wake, Katibu wa Mgodi wa Kasi Mpya, Hosea Mbusule, alisema kuwa transfoma iliyopo haina uwezo wa kuendesha mashine zote, na mara kadhaa wamekuwa wakikumbwa na matatizo ya kukatika kwa umeme hali inayosababisha kusimama kwa shughuli za uzalishaji au kutumia majenereta mbadala.
Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, alisema serikali itahakikisha migodi yote midogo isiyokuwa na nishati ya umeme inapatiwa huduma hiyo kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija kwa wachimbaji. Aidha, aliwataka viongozi wa migodi kushirikiana na serikali kudhibiti utoroshaji wa madini ili kuepusha upotevu wa mapato ya taifa.
“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tayari ametoa fedha nyingi kuboresha sekta mbalimbali, ikiwemo miundombinu na huduma za umeme. Tutakapofanikisha kufikisha umeme migodini, uchumi wa wachimbaji utaimarika, na serikali itapata mapato yake ipasavyo,” alisema Mhita.
Kuhusu miundombinu ya barabara inayotumiwa kufika migodini na kusafirisha mawe yenye madini, Mhita alisema atatoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kufika eneo hilo na kutatua changamoto hiyo, akisisitiza kuwa fedha tayari zimetolewa na Rais Samia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED