Viongozi wastaafu Afrika waja na wito wa mazingira

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 08:22 PM Apr 09 2025
Viongozi wastaafu Afrika waja na wito wa mazingira
Picha: Mpigapicha Weu
Viongozi wastaafu Afrika waja na wito wa mazingira

VIONGOZI wastaafu Afrika pamoja na wataalamu wa maendeleo wametoa wito kwa serikali barani humo, kutekeleza mikakati inayotambua na kutoa motisha kwa watu wanaowekeza katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Wito huo umetolewa jana nchini Uganda katika siku ya pili ya Mkutano wa 8 wa Viongozi wa Afrika (ALF), unaoendelea chini ya uratibu wa Taasisi ya Uongozi.

Mlezi wa Kongamano hilo na Rais wa Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amesisitiza umuhimu wa mataifa ya Afrika kuwawezesha wananchi wao, hususan wataalamu wa  majadiliano wa masuala ya mazingira, ili waweze kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kimataifa.

“Tunaponyimwa fursa ya kutumia ipasavyo rasilimali zetu na badala yake zikanufaisha mataifa yenye nguvu kiuchumi, tunajikuta tukikosa uwezo wa kushughulikia changamoto kama mabadiliko ya tabia nchi na uhifadhi wa misitu,” amesema Kikwete.

Ameongeza kuwa, “Tunatoa motisha kwa watu wanaopanda miti mipya, lakini hatuwatambui wala kuwathamini wale wanaolinda misitu iliyopo. Hii inaleta pengo kubwa katika juhudi za uhifadhi na kudhoofisha azma ya kulinda ikolojia ya asili.”

Viongozi wastaafu Afrika waja na wito wa mazingira
Kikwete amesisitiza kuwa mfumo wa sasa ambao unamnufaisha kifedha mharibifu wa mazingira huku mhifadhi akikosa chochote, hauwezi kudumu. “Ni lazima tubadilishe mtazamo huu kwa kutambua mchango wa misitu katika kuhifadhi kaboni, na kuwazawadia wanaojitolea kuilinda,” amesema,

Naye Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia na Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo, Hailemariam Desalegn Boshe, ameeleza kuwa uhaba wa fedha za Mabadiliko ya tabia nchi ni kikwazo kikubwa kwa Afrika kunufaika ipasavyo na fursa za uhifadhi wa mazingira.

“Ni muhimu tuwe na mshikamano na tushirikiane kama bara katika majadiliano ya kimataifa ili kuhakikisha tunapata manufaa halisi kutoka kwenye biashara ya uhifadhi wa misitu,” amesema Boshe.

Amehimiza nchi za Afrika kuunda timu thabiti za Majadiliano zitakazotetea kwa nguvu maslahi ya bara katika mikutano ya kimataifa kuhusu mazingira.
Viongozi wastaafu Afrika waja na wito wa mazingira
Mkurugenzi mwanzilishi wa shirika la CORDIO Afrika Mashariki, Dk. David Obura, akizungumzia umuhimu wa maboresho katika sheria za tabianchi ili kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya uhifadhi wa misitu.

“Kwa sasa tunahitaji kujenga mifumo imara ya fedha za tabianchi itakayovutia uwekezaji katika sekta ya mazingira, hasa uhifadhi wa misitu,” amesema Dk. Obura.

Naye Profesa Chukwumerije Okereke, mtaalamu wa utawala wa tabianchi na sera za umma kutoka Chuo Kikuu cha Bristol, akiwasilisha mapendekezo matano muhimu Ambayo ni kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za tabianchi, kuwekeza kwenye maeneo yenye thamani kubwa ya kiuchumi, kutumia suluhisho za ndani, kusisitiza haki ya tabianchi, na kufafanua upya dhana hiyo ili iwe na muktadha wa Kiafrika.

Profesa Okereke amebainisha kuwa licha ya hatua zilizopigwa, bara la Afrika bado linakabiliwa na pengo la kifedha linalokadiriwa kuwa dola bilioni 2.8, linalozuia juhudi za uendelezaji wa uhifadhi wa mazingira.