WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya afya nchini, yamechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi na kuimarisha pia utalii wa tiba.
Pia Waziri Majaliwa amesema kufikia Februari mwaka huu, wagonjwa 7,843 kutoka nje ya nchi wametibiwa nchini ikilinganishwa na wagonjwa 5,705 wa mwaka 2020.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya ofisi ya waziri mkuu na Bunge leo Waziri Majaliwa amesema ushirikiano wa serikali na sekta binafsi yamechochea mafanikio na umewezesha kuongezeka kwa vituo vya huduma za afya nchini kutoka 8,458 mwaka 2020 hadi 9, 826, Februari, mwaka huu.
“Kutokana na jitihada hizo vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2020 hadi 104 Februari mwaka huu, na vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 67 mwaka 2020 hadi 43 Februari mwaka huu,” amesema Waziri Majaliwa.
Kadhalika, ameeleza kuwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zimeendelea kuimarika ambako kwa sasa zinapatikana kwenye hospitali za rufaa za mikoa zinazotoa huduma nane za kibingwa, na kwamba awali zilikuwa zinapatikana katika ngazi ya Kanda.
“Huduma hizo za matibabu ni pamoja na afya ya uzazi na magonjwa ya wanawake, afya ya watoto, magonjwa ya ndani, upasuaji, upasuaji wa mifupa na ajali, huduma za dharura, huduma za mionzi, huduma za ganzi na dawa za usingizi,” amesema Majaliwa.
Pia Waziri Majaliwa amesema upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya kisasa na bidhaa za afya nchini vimeimarika kutoka asilimia 73 mwaka 2020 hadi 89.3 Februari mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED