Samia aandika historia Angola, atetea mshikamano wa Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:29 PM Apr 09 2025
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema bara la Afrika linahitaji kuwa na mshikamano wa pamojan ili liweze kuwa imara na kuheshimika..

Alisema hayo wakati akilihutubia Bunge la Angola akiweka historia ya kuwa rais wa kwanza mwanamke kulihutubia bunge hilo.

"Giza linaloonekana katika bara letu ni kielelezo kuwa tunahitaji kuwa na mshikamano utakaozifanya nchi zetu kuwa imara" alisema.

Alisema mshikamano utakaooneshwa nwa nchi za bara hilo, sio tu utapambana na umaskini bali pia utalifanya Bara la Afrika kuheshimika.

Rais Samia alihutubia bunge hilo akiwa katika siku ya pili ya ziara yake nchini humo, baada ya kupewa heshima ya kulihutubia na Rais wa Bunge wa nchi hiyo ambaye pia ni mwanamke, Caroline Carqueira.

Aidha, Rais Samia alisema yeye pamoja na rais mwenzake wa Angola, Joao Goncalves Lourenco wamekubaliana kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kuwa changamoto zinazozikumba nchi hizo mbili zikiwamo za kuimarisha uchumi wanapambana nazo ili kuleta maendeleo si ya nchi hizo tu bali kwa bara zima la Afrika.

Alimpongeza Rais Lourenco.kwa kuimarisha uchumi wa nchi yake na kupambana na rushwa na kuwataka wananchi wa nchi hiyo kuendelea kumuunga mkono rais wao katika mapambano hayo.

Uchumi wa Angola unafikia Dola za Kimarekani bilioni 100 na kulifanya taifa hilo kuwa na uchumi imara unaotokana na biashara ya mafuta na madini.

Ziara ya Rais Samia nchini Angola ni ya kuimairisha uhusiano wa nchi hizo mbili uliojengwa na waasisi Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Hayati Agustino Neto wakati wa harakati za ukumbozi wa nchi ya Angola.

Rais Samia ametembelea nchi hiyo baada ya kupita miaka 19 tangu Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipotembelea nchi hiyo mara ya mwisho mwaka 1996.

Alisema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji na kuwakaribisha wananchi wa nchi hiyo kuitembelea na Watanzania kutafuta fursa Angola.

Alisema Tanzania ina hazina kubwa ya gesi na madini ambayo bado haijatumika vya kutosha.

Alimpongeza Spika wa Bunge, Caroline kwa kuwa mfano mzuri wa kuliendesha bunge lake kidemokrasia.

Aliahidi kuwa katika ziara yake ambayo ameambatana na baadhi ya wabunge itaendeleza uhusiano wao wa kutembeleana na anawaruhusu kufanya hivyo.

Aidha, alisema Tanzania kiihitoria ilisimama imara kuithamini Angola kwa juhudi zake za kupambana na utawala wa kikoloni ndio maana kuna baadhi ya maeneo yamepewa majina ya wapigania uhuru wake.

Hata hivyo, alisema nchi za Afrika bado zinachangamoto ya ulinzi na usalama na kwamba ndio maana katika hati za makubaliano walizotia saini juzi suala la usalama limepewa kipaumbele.