Simba yatinga nusu fainali CAF, yaikacha 'Mwakarobo'

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:10 AM Apr 10 2025
Simba yatinga nusu fainali CAF, yaikacha 'Mwakarobo'
Picha: Mpigapicha Wetu
Simba yatinga nusu fainali CAF, yaikacha 'Mwakarobo'

Simba imetinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF baada ya kuiondoa Al Masry ya Misri kwa mikwaju ya penati 4-1 kwenye mchezo pili wa robo fainali uliofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza kule Misri, Simba ilikubali kipigo cha mabao 2-0, ambapo Jijini Dar es Salaam Simba ilirejesha mabao hao, kupitia kwa Elie Mpanzu na Steven Mukwala. 

Shomari Kapombe alifunga penati ya ushindi huku Mlinda mlango Moussa Camara akiibuka nyota wa mchezo wa kuokoa mikwaju miwili ya penati. 

Kabla ya Mchezo wa leo, simba ilikuwa inaitwa mwakarobo na watani zao Yanga kwa kushindwa kuvuka robo fainali mara kwa mara. Kati ya robo fainali 7 kabla ya hii ya sasa, ilikuwa imefanikiwa kuvuka mara mbili tu hatua hiyo. 

JINA MWAKAROBO. 

Tangu kuanzishwa kwa Simba mwaka 1936, imewahi kufika robo fainali ya mashindano ya Afrika mara nane, kwenye michuano mbalimbali ikiwemo Kombe la Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), Kombe la CAF, na Kombe la Shirikisho. Cha kushangaza, katika mara hizo zote nane, ilikuwa imevuka hatua ya robo fainali mara mbili tu. 

Mara ya kwanza kilikuwa mwaka 1974, Simba ilipowatoa Hearts of Oak ya Ghana kwa jumla ya mabao 2-0 ugenini mjini Accra, Ghana kwa mabao ya Abdallah 'King' Kibadeni na Adam Sabu, kabla ya Kwenda sare tasa ya 0-0 jijini Dar es Salaam. Kikosi cha Simba kilikuwa na magwiji kama 'King' Kibadeni, Sabu, Mohamed Kajole, Athuman Mambosasa, na Abbas Dilunga. Hii ilikuwa ni enzi ambazo hata mfadhili mkubwa wa sasa wa klabu, Mohammed "Mo" Dewji, alikuwa hajazaliwa. 

Hata hivyo, katika hatua ya nusu fainali, Simba walikumbana na Mehala El Kubra ya Misri na kupoteza nyumbani 1-0 na kisha kipigo kama hicho ugenini na kuondolewa kwa jumla ya mabao 2-0. 

Simba ilivuka tena robo fainali mwaka 1993, safari hii dhidi ya Al Harrach ya Algeria. Iliibuka na ushindi wa 3-0 nyumbani kwa mabao mawili kutoka kwa Edward Chumila "Edo" na moja kutoka kwa Ramadhani Abdul "Mashine", kabla ya kupoteza 2-0 ugenini. Hii ilikuwa enzi ambazo msemaji wa sasa wa klabu, Ahmed Ally, alikuwa bado mtoto wa darasa la kwanza au pili au hajaanza shule kabisa.

Baada ya hapo, Simba iliitoa Atletico Sport Aviacao ya Angola nusu fainali na kufika fainali, ambako walikumbana na Stella Abidjan ya Ivory Coast na kupoteza jumla ya mabao 2-0. 

Hizi ndizo nusu fainali mbili pekee ambazo Simba imewahi kuzifikia kwa karne karibu tisa tangu kuanzishwa kwake. Mara nyingine zote, hatua ya robo fainali imekuwa kama ukuta wa chuma. 

Katika Kombe la Klabu Bingwa Afrika (zamani), Simba ilishiriki mara 9 na kufika robo fainali mara mbili, mwaka 1974 walipovuka na 1994 walipoishia hapo. 

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo ni toleo jipya la mashindano hayo, Simba wameshiriki mara 9 pia, na kufika robo fainali mara nne, katika misimu ya 2018/2019, 2020/2021, 2022/2023, na 2023/2024, lakini bila kuvuka Kwenda nusu.
 

Katika Kombe la Shirikisho la CAF, Simba wameshiriki mara 7 hadi sasa, na hii ya 2024/2025 ni robo fainali yao ya pili katika michuano hiyo, baada ya ile ya 2021/2022. 

Licha ya rekodi hiyo ya kukwama kufika robo fainali mara kwa mara, tangu mwaka 2018 hadi sasa, Simba SC imefanikiwa kuwa klabu yenye mafanikio makubwa zaidi kimataifa kutoka Afrika Mashariki kwa kufika robo fainali sita katika mashindano makubwa barani Afrika.

Kwa kiwango hicho, bila shaka Simba ni mabingwa wa kweli wa ukanda huu. Kwa rekodi ya kufika robo faibali, simba inastahili sifa, ni hatua kubwa imepiga katika miaka ya hivi karibuni. Watani zao Yanga wao wanajivunia kuingia fainali ya kombe la shirikilo, CAF, msimu wa 2022/2023.

Lakini mashabiki wa Simba hawatosheki na robo fainali tu. Walikuwa wanataka hatua kubwa zaidi. Na sasa jina la Mwakarobo linaweza kuwa historia kwao.

 
#Historia na BBC