Serikali imeanza rasmi kutoa mafunzo kwa walimu 4,000 wa shule za msingi na sekondari ili kuwawezesha kutambua mapema dalili za usonji (Autism Spectrum Disorders - ASD) kwa watoto, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya ya akili kwa watoto nchini.
Akizungumza Jumatano wiki hii katika Kongamano la 13 la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza na Afya ya Akili kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Omary Ubuguyu, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa majaribio wa mwaka mmoja unaotekelezwa katika shule 100 jijini Dar es Salaam.
“Mafunzo haya yanawapa walimu maarifa ya kutambua dalili za usonji mapema, ili watoto wapate huduma stahiki kwa wakati. Walimu wana nafasi ya kipekee kwani watoto wengi hutumia muda mwingi shuleni kuliko hospitalini,” alisema Dk. Ubuguyu.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, na Taasisi ya Lukiza Autism Foundation. Dk. Ubuguyu alibainisha kuwa uelewa mdogo miongoni mwa walimu umechangia watoto wengi wenye usonji kutotambuliwa mapema, hivyo kukosa msaada wanaohitaji.
Katika kongamano hilo, pia kulizinduliwa kitabu kipya kwa jina la "Autism Spectrum Disorders and Related Conditions: A Comprehensive Guide for Medical Professionals & Parents", ambacho kinatoa mwongozo kwa wataalamu wa afya na wazazi kuhusu huduma bora kwa watoto wenye usonji.
Akichangia mjadala huo, Profesa Karim Manji alisema kuwa takwimu zinaonyesha mtoto mmoja kati ya 150 huzaliwa na hali ya usonji, lakini ni nusu tu ya Watanzania wanaofahamu kuhusu tatizo hilo.
“Tunahitaji kufanya shule ziwe jumuishi zaidi, kuhakikisha watoto wote wanapimwa katika vituo vya afya, na kuingiza huduma za usonji katika mipango ya afya ya umma. Pia tunapaswa kudhibiti vituo vinavyotoa huduma hizi ili kuhakikisha viwango bora vinazingatiwa,” alisema Prof. Manji.
Alisisitiza kuwa usonji si suala la kitabibu pekee, bali pia ni la kijamii, kiuchumi na haki za binadamu.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema kuwa katika miaka minne iliyopita, chuo hicho kimeanzisha programu mbalimbali zikiwemo tiba ya viungo, famasia, udaktari, pamoja na tiba ya lugha na kusema.
“Hadi sasa, zaidi ya wanafunzi 200 wamejiunga na programu hizo, hatua inayosaidia kuongeza idadi ya wataalamu watakaosaidia kukabiliana na changamoto za afya ya akili, ikiwemo usonji,” alisema Prof. Kamuhabwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED