Wizara yatoa fursa kubadili tahsusi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:22 PM Apr 03 2025
Fursa yatolewa kubadili tahsusi
Picha: Mtandao
Fursa yatolewa kubadili tahsusi

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imetoa siku 30 za kubadilisha machaguo ya tahasusi kwa wahitimu wa kidato cha nne kwa mwaka 2024, ili kuwezesha kuchaguliwa masomo yatakayowaandaa kuwa na utaalamu stahiki.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, amesema hatua hiyo ni maandalizi ya kufanya uchaguzi wa wanafunzi kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya kati na ufundi vya serikali kwa Mwaka 2025 na ubadilishaji huo utafanyika kwa njia ya mtandao kuanzia Machi 31 hadi Aprili 30, mwaka huu.

Amesema serikali imekuwa ikitoa fursa, kwa wahitimu hao kufanya mabadiliko ya tahsusi na kozi mbalimbali walizochagua kupitia fomu ya uchaguzi, ili kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu wao.

Ameelekeza kuwa wanaotaka kubadili machaguo wanatakiwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Student Selection MIS), unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz.