Serikali yakusanya bil 755/- za madini

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 03:40 PM Apr 03 2025
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (kushoto) akiwa ameongozana na baadhi ya maofisa wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya kukagua eneo la uwekezaji wa kiwanda cha kuchenjua shaba cha MAST
Picha: Nerbart Msokwa
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (kushoto) akiwa ameongozana na baadhi ya maofisa wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya kukagua eneo la uwekezaji wa kiwanda cha kuchenjua shaba cha MAST

SERIKALI imekusanya zaidi ya Sh. bilioni 755 kutoka kwenye sekta ya madini kuanzia Julai, mwaka jana mpaka sasa, ambazo zimeingizwa kwenye mfuko mkuu hali ambayo inaashiria kuendelea kukua kwa sekta hiyo.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameyasema hayo wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya, alipofanya ziara ya kukagua Mtambo wa Kuchenjua madini ya Shaba wa Kampuni ya MAST ambao ni wa kwanza kujengwa wilayani humo.

Amesema kiwango hicho cha fedha kilichokusanywa kimeshavuka lengo la mwaka wa fedha 2023/2024 ambao zilikusanywa Sh. bilioni 703.

Amesema ongezeko la ukusanyaji wa mapato hayo limetokana na serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji ambayo yamesababisha wawekezaji wengi wa ndani na wa nje kujitokeza kuwekeza kwenye sekta hiyo.

Vilevile amesema ongezeko hilo, limetokana na serikali kuanzisha masoko maalumu ya kuuzia madini kwenye mikoa mbalimbali, hali ambayo imesababisha mauzo kupita kwenye mfumo maalumu.

“Lakini pia kumekuwa na ongezeko la sekta hii kuchangia kwenye pato la taifa, kabla ya kuanzishwa masoko sekta hii ilikuwa inachangia asilimia saba pekee, lakini kwa sasa tumefikia asilimia zaidi ya tis ana tunatarajia kufikia asilimia 10,” amesema Mavunde.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (wa nne kushoto mwenye kofia nyeusi) akiwa ameongozana na baadhi ya maofisa wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya kukagua eneo la uwekezaji wa kiwanda cha kuchenjua shaba cha MAST
Waziri Mavunde ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wa kiwanda hicho, akidai kuwa kitaongeza uzalishaji wa madini hayo, kuongeza ajira kwa wananchi pamoja na kukuza Pato la Taifa.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mhandisi Geofrey Kente amesema ilianza kufanya utafiti wa madini hayo mwaka 2011, lakini kwa sasa imeshaanza uzalishaji kwa majaribio.

Amesema mpaka sasa kampuni hiyo imeshazalisha tani 14 za shaba zenye asilimia 70 na kwamba wanatarajia kuzindua rasmi mtambo huo Julai, mwaka huu.

Amesema mbali na kujenga mtambo huo katika wilaya ya Chunya, pia wanakusudia kujenga mitambo mingine kwenye mikoa ya Dodoma, Ruvuma, Pwani na Mtwara ambako pia wamefanya utafiti.

“Awali tulipata upinzani mkubwa kwa sababu wananchi wa huku Chunya walikuwa wanafikiria dhahabu pekee, kwa sasa tumeshawekeza zaidi ya Dola za marekani Milioni tatu,” amesema Mhandisi Kente.

Amesema kampuni hiyo imeajiri wafanyakazi 104 ambao asilimia 99 ni Watanzania na kwamba wawili pekee ni raia wa nchi ya Zambia, ambao wameajiriwa kwa ajili ya kusaidia kwenye uzoefu wa ujenzi wa mitambo hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bosco Mwanginde, amesema kwa sasa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi, ili wawe na uelewa wa madini hayo na kuacha kufikiria dhahabu pekee.

Amesema uwekezaji uliofanywa na kampuni hiyo umesaidia kuongeza mapato kwa wananchi wa Kata ya Mbugani, ambako mwekezaji amewekeza kutokana na kuwa na soko la uhakika la mazao yao pamoja na nyumba zao kupata wapangaji.

0-0000