Tabibu asimamishwa kazi kupisha uchunguzi tuhuma kifo cha mgonjwa

By Stevie Chindiye , Nipashe
Published at 05:18 PM Apr 03 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, Chiza Marando.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, Chiza Marando.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, Chiza Marando, amemsimamisha kazi Afisa Tabibu wa Zahanati ya Kijiji cha Marumba, Kata ya Marumba, Ignas Yustine Magomba, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za uzembe kazini, zinazohusiana na kifo cha mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Zainabu Kazembe Boma.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Marando alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa kufuatia malalamiko kutoka kwa familia ya marehemu, ambao hawakuridhishwa na huduma alizopatiwa ndugu yao kabla ya kufariki dunia. Malalamiko hayo, ambayo yamesambaa pia katika mitandao ya kijamii, yanadai kuwa kulikuwa na uzembe katika utoaji wa huduma za afya kwa marehemu.

Marando alibainisha kuwa uchunguzi wa kina utafanyika ili kubaini ukweli wa madai hayo. Aliongeza kuwa iwapo itathibitika kuwa kulikuwa na uzembe, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.

"Hatutasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kufanya uzembe na kukiuka maadili ya kazi," alisisitiza Marando.

Aidha, Mkurugenzi huyo aliwataka watumishi wa umma, hususan wa sekta ya afya, kuhakikisha wanatoa huduma kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi.

Pamoja na hayo, Marando alitoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Tunduru kujenga utamaduni wa kutoa taarifa za malalamiko yao mapema kwa mamlaka husika pindi wanapokumbana na changamoto katika upatikanaji wa huduma za kijamii, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.