Milioni 255.8/- zawaondoa kwenye ‘kausha damu’

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:12 PM Apr 03 2025
Baadhi ya wanufaika wa mikopo
Picha: Marco Maduhu
Baadhi ya wanufaika wa mikopo

HALMASHAURI ya Manispaa ya Shinyanga, imetoa Sh. milioni 225.8 fedha za mikopo kwa asilimia 10 kwa vikundi 19.

Fedha hizo zimetolewa Aprili 2, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Peres Kamugisha, akisoma taarifa ya utoaji wa mikopo hiyo, amesema wametoa fedha hizo ni kwa wanawake kwa vikundi 11, vijana vikundi saba na kikundi kimoja cha watu ulemavu.

“Mikopo hii ya asilimia 10 ni endelevu na itaendelea kutolewa kwa vikundi ambavyo vitakidhi kanuni na taratibu zilizopo,” amesema Peres.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kwa utoaji wa mikopo hiyo, huku akivisisitiza vikundi ambavyo vimepewa mikopo, kuwa waitumie kwa madhumuni kusudiwa pamoja na kuirejesha kwa wakati.

“Ninawasisitiza wanavikundi ambao mmepata mikopo hii mkaitumie kwenye miradi ambayo mliiorodhesha kipindi mnaomba mikopo na msijaribu kuzitumia fedha ambazo mmepata kwenye miradi mingine ambayo hamkuiorodhesha, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha kanuni na taratibu,” amesema Mtatiro.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo, akiwamo Penina Ezekiel, ameishukuru serikali kwa utoaji wa mikopo hiyo, ambayo wamesema itawasaidia kuondokana na mikopo kausha damu, na kwamba wataitumia vizuri, ili wajikwamua kiuchumi.