MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imetoa msaada wa mahitaji mbalimbali katika vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, ili kusherehekea sikukuu Eid el Fitri na Pasaka.
Vituo vilivyonufaika na msaada huo, Dar es Salaam ni Umra Orphanage Center kilichopo Magomeni Mikumi na Mother of Mercy Children’s Home, kilichopo Madale.
Pia, mamlaka imetoa misaada hiyo katika mikoa yote ya Tanzania.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amewashukuru walezi wa vituo hivyo, kwa kazi wanayoifanya ya kuwalea watoto na kuwasomesha hadi kufikia hatua ya kuajiriwa.
"Mahitaji haya tunayatoa katika mikoa yote nchini, tumebaini maeneo yenye uhitaji ni mengi, hivyo hii ni kama njia ya kurudisha kwa jamii, mamlaka hii ni ssehemu ya jamii na inaguswa na changamoto za watoto hawa,” amesema Kamishna Mwenda.
Ameendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuchangia maendeleo ya nchi kwa kulipa kodi, akieleza kuwa mapato yanayokusanywa yanasaidia serikali kutoa huduma muhimu kwa jamii.
Katika hatua ya kuonesha mchango wake binafsi, Kamishna Mwenda ameahidi kutoa shilingi milioni nne kusaidia upatikanaji wa bima ya afya, kwa watoto wa Umra Orphanage Center.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano TRA, Richard Kayombo, pamoja na Naibu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Nahoda Nahoda, wamekabidhi msaada kwa kituo cha Mother of Mercy Children’s Home.
Kayombo amewatia moyo watoto wa kituo hicho na kuahidi kuwa TRA itaendelea kushirikiana nao. Amebainisha kuwa TRA inatambua umuhimu wa kusaidia makundi yenye uhitaji na itaendelea kutoa mchango wake kwa jamii.
Kwa upande wao, Muasisi wa Umra Orphanage Center, Rahma Kishumba na msimamizi wa Mother of Mercy Children’s Home, Sister Christina Christopher, waliishukuru TRA kwa msaada huo.
Msaada huo unaonesha dhamira ya TRA katika kusaidia jamii na kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanapata mahitaji ya msingi, hasa katika kipindi cha sikukuu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED