Tabora United: Hatuihofii Yanga

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 02:28 PM Apr 01 2025
Msemaji wa klabu hiyo, Christina Mwagala
Picha: Mtandao
Msemaji wa klabu hiyo, Christina Mwagala

KLABU ya Tabora United imesema wapo tayari kuwakabili Yanga kwenye mchezo wao leo na hawaihofii kwa kuwa mpira ni dakika 90.

Akizungumza na Nipashe jana, Msemaji wa klabu hiyo, Christina Mwagala, alisema wamefanya maandalizi ya kutosha na watafanya kama kile walichokifanya kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza walioibuka na ushindi wa mabao 3-1. 

"Baada ya kushindwa kusonga mbele katika mashindano ya Kombe la FA hatuna kingine zaidi ya kufuta machozi yetu kwa kuifunga Yanga kwenye mchezo wetu waLigi Kuu, tupo tayari kuwakabili na hawatupi hofu yoyote," alisema Mwagala.

Alisema wanaupa umuhimu mchezo huo wa leo kwa kuwa wana lengo la kupata pointi tatu na kuwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani. 

Alisema makosa ambayo yalijitokeza kwenye michezo iliyopita benchi la ufundi limefanyia kazi na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo wa leo.

"Kikubwa tutachukua tahadhari kubwa kwenye mchezo huu, kikubwa tunataka ushindi," alisema.

Mchezo huo leo unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka hasa kutokana na kile Tabora United walikifanya kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa kushtukiza Yanga na ushindi wa mabao 3-1.